Iran: Mkataba wa Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan unaonyesha kuongezeka hali ya kutoaminika ahadi za usalama za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140574-iran_mkataba_wa_saudi_arabia_uturuki_na_pakistan_unaonyesha_kuongezeka_hali_ya_kutoaminika_ahadi_za_usalama_za_marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anasema makubaliano ya ulinzi yaliyosainiwa hivi karibuni kati ya Saudi Arabia, Pakistani na Uturuki yanaonyesha mtazamo wa mataifa ya kikanda kuhusu "udanganyifu" wa Marekani linapokuja suala la usalama.
(last modified 2026-08-11T03:24:11+00:00 )
Aug 11, 2026 03:22 UTC
  • Esmaeil Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
    Esmaeil Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anasema makubaliano ya ulinzi yaliyosainiwa hivi karibuni kati ya Saudi Arabia, Pakistani na Uturuki yanaonyesha mtazamo wa mataifa ya kikanda kuhusu "udanganyifu" wa Marekani linapokuja suala la usalama.

Esmaeil Baqaei alitoa matamshi hayo jioni ya jana katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran akijibu swali kuhusu msimamo wa Iran juu ya mkataba wa pande tatu, unaojulikana kama Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa Makka.

Amesema tukio hilo linaonyesha mabadiliko katika mtazamo wa nchi za kanda hii linapokuja suala la usalama.

"Kutokana na matukio ya kipindi cha miaka miwili au mitatu iliyopita, nchi za kikanda zimegundua kuwa usalama si bidhaa inayoweza kununuliwa kutoka kwa madalali bandia wa usalama," aliongeza Baqaei.

Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zilisaini Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa Makka Ijumaa iliyopita kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa pamoja dhidi ya kitendo chochote cha uchokozi.

Katika taarifa ya pamoja, waliotia saini mkataba huo walisema kwamba shambulio la kutumia silaha dhidi ya mojawapo ya nchi hizo tatu litatambuliwa kama shambulio kwa wote.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa mkataba huo unalenga kuimarisha usalama wa pamoja na kukuza amani, usalama na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia na kwingineko.

Baqaei amepuuza wasiwasi kuhusu makubaliano hayo ya ulinzi, akisisitiza kwamba Tehran ina "uhusiano mkubwa" na nchi hizo tatu.

"Tunadumisha uhusiano wa karibu na Pakistan, Uturuki na hata Saudi Arabia na hakuna sababu ya Iran kuwa na wasiwasi kuhusu mkataba huo," amesema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.

Amesisitiza kwamba uhusiano wa kitamaduni uliokita mizizi kati ya watu wa Iran, Pakistan na Uturuki uko "wazi kabisa."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa; "Matukio haya yanaonyesha kwamba nchi za kanda hii haziwezi kuamini madai ya Marekani na nchi zingine za nje ya kanda ya kulinda usalama."

Esmaeil Baqaei pia amesema Tehran na Muscat zimekubaliana kuhusu njia ya urambazaji kupitia Lango-Bahari la Hormuz na zinachunguza baadhi ya vipengele vya kiufundi vinavyohusiana na mpango huo.

Ameongeza kuwa Iran itaanzisha mifumo ya kufuatilia usafirishaji katika njia hiyo ya kimkakati ya majini na pia itatoa huduma kwa vyombo vinavyotumia njia hiyo kama sehemu ya juhudi za kuhakikisha urambazaji salama.

Baqaei amesema Tehran kwa sasa haishiriki katika mazungumzo na Washington lakini badala yake inafanya mazungumzo na Oman ili kuainisha njia ya meli kupitia Lango-Bahari la Hormuz.