Araqchi: Iran ilifanikiwa katika nyanja zote mbili, yaani vita na diplomasia dhidi ya uchokozi wa Marekani na Israel
-
Abbas Araqchi (Kushoto pichani)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi ameeleza kuwa Tehran imepata ushindi katika nyanja zote mbili za kijeshi na kidiplomasia katika uchokozi wa hivi karibuni wa Marekani na Israel katika vita vya siku 12 na kusisitiza kuwa muqawama wa Iran uliwalazimisha maadui kuomba kufanya mazungumzo.
Akizungumza leo katika hafla ya kutia saini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya sekta ya diplomasia na afya kwa ajili ya ujenzi mpya wa miundombinu iliyoharibiwa wakati wa vita vya hivi karibuni, Araqchi amesema: Vita vya siku 12, kama ilivyokuwa kwa vita vya miaka nane kati ya Iran na Iraq, vilishuhudia "matukio yasiyo na kifani" ya ushujaa na kujitolea kwa Wairani katika sekta zote.
Ameongeza kuwa jitihada za wanaume na wanawake wa Iran zilihakikisha kuwa maisha na riziki za watu, pamoja na upatikanaji wa huduma za afya na matibabu haviathiriki wakati wa uvamizi huo.
"Iran imelifanya jeshi kubwa zaidi duniani lishindwe kufanya lolote na imelishinda. Hii si kaulimbiu; ni hali halisi ya mambo. Jamhuri ya Kiislamu imeudhihirishia ulimwengu kuwa ni nguvu imara na yenye uwezo mkubwa," ameeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.
Sayyid Araqchi amesema: Amesikia mara kwa mara Mawaziri wa Mambo ya Nje na maafisa wakisifu utendaji wa Iran wakisema Wairani wameishangaza dunia kwa kukabiliana na Marekani, Israel, nchi za Magharibi na waungaji wao mkono.
Araqchi amesema, hakuna aliyedhani kuwa Iran ingeweza kusimama kidete kwa namna hii, na hatimaye kuwalazimisha maadui kuomba kufanya mazungumzo.