Rezaei: Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa ikiwa tu US itayakubali masharti ya Iran
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema, kufunguliwa tena kikamilifu Mlango-Bahari wa Hormuz katika Ghuba ya Uajemi, ambao umewekewa vizuizi vya uvukaji na Iran tangu mwanzoni mwa mwezi Machi kutokana na uchokozi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel kutafanyika pale tu Marekani itakapoyakubali masharti ya Iran.
Mohsen Rezaei, Katibu mpya wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa (SNSC) amemueleza Balozi wa China mjini Tehran Zong Piyu kwamba Marekani lazima ikomeshe vita dhidi ya Iran na washirika wake wa kikanda na kuachilia fedha za Iran zilizozuiliwa ili mlango bahari wa Hormuz ufunguliwe tena kikamilifu.
"Madamu Marekani haibadilishi mwenendo wake na kukubali masharti ya Iran, Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa," amesisitiza Rezaei katika mkutano huo.
Amesema pia kwamba, katika wiki zilizopita, Iran iliwasilisha masharti mengine kwa Marekani kupitia wapatanishi, ambao wamehusika katika mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili.
Rezaei amesisitiza kuwa, hata kama Iran na Oman zitafikia makubaliano kuhusu njia za usafiri zitakazotumika katika njia ya majini ya Mlango-Bahari wa Hormuz, makubaliano hayo hayatakuwa na athari yoyote kwa uamuzi wa Iran wa kuufunga au kuufungua tena mlango-bahari huo.
Wakati huohuo, Katibu huyo wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameweka ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X kuhusiana na kadhia ya Mlango-Bahari wa Hormuz akisema: "Ujumbe wa IRAN uko wazi: Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa tena hadi Marekani itakapohitimisha vita na mzingiro wa baharini, itakapoachilia mali za Iran zilizozuiliwa, na ikakubali kusitishwa mapigano katika eneo lote, ikiwa ni pamoja na Lebanon na Ghaza."
Rezaei amesisitiza katika andiko hilo kwamba: "Mlango-Bahari utabaki umefungwa, hadi pale masharti yote yatakapotimizwa"…/