Rais wa Iran amwambia Waziri Mkuu wa Japan: Iran haijawahi kukiuka sheria za kimataifa
-
Pezeshkian kwa Japan: Iran haijawahi kukiuka sheria za kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa Iran haijawahi kukiuka sheria za kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dkt. Masoud Pezeshkian ameyasema hayo Jumatano katika mazungumzo ya simu na Bi. Sanae Takaichi, Waziri Mkuu wa Japan kuwa. Amemfahamisha bayana kuwa Iran haijawahi kamwe kutaka kuvuruga utulivu katika eneo la Asia Magharibi. Amesema kinyume chake, ni Marekani na utawala wa Kizayuni ndio waliovuruga amani na utulivu kwa kufanya uchokozi dhidi ya Iran na kumuua shahidi kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika mazungumzo hayo, Rais Pezeshkian amepongeza mitazamo chanya ya Japan kuhusu haja ya kusitisha vita. Amesisitiza kuwa Iran haikutaka hata kidogo kuleta machafuko, na kwamba ni Marekani na utawala wa Kizayuni ambao kwa uchokozi wao dhidi ya Iran, mauaji ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mauaji ya raia wengi wasio na hatia, wakiwemo wanafunzi wa shule mjini Minab, pamoja na uharibifu wa miundombinu ya kiraia, wamekuwa sababu kuu ya kuvurugika kwa amani na utulivu katika eneo hili.
Rais amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kutenda nje ya mfumo wa sheria za kimataifa na imekuwa ikijitahidi daima kuimarisha uhusiano mwema na majirani zake. Rais aidha ameelezea matumaini yake kuwa juhudi za kidiplomasia za Japan katika kurejesha amani na utulivu zitaleta matunda na kuzuia jinai na uchochezi wa vita unaofanywa na madola hayo vamizi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Japan amesisitiza uungaji mkono wa Tokyo kwa njia za kidiplomasia ili kuhitimisha vita, akieleza kuwa hatua hiyo inalingana na maslahi ya muda mrefu ya Iran na ya kanda nzima.
Bi. Takaichi amekaribisha maendeleo ya mazungumzo kati ya Iran na Oman kuhusu Lango la Hormuz, na ametoa wito wa kufanikisha mazungumzo hayo ili njia hiyo ya usafirishaji ifunguliwe haraka iwezekanavyo.
Aidha, Waziri Mkuu wa Japan amemwomba Rais wa Iran kutumia ushawishi wa Tehran kuzuia kuongezeka kwa mivutano katika lango la Bab al-Mandab.
Katika mazungumzo hayo ya simu, viongozi wa nchi hizo mbili walisisitiza azma yao ya kuendeleza mazungumzo na kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya mataifa yao mawili.