Mkuu wa Idara ya Mahakama amwambia Trump: Iran ndiyo mmiliki na mtawala wa Lango la Hormuz
-
Gholam-Hossein Mohseni-Eje’i
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam-Hossein Mohseni-Eje’i, amezitaja kauli za hivi karibuni za Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu umiliki wa Lango Bahari la Hormuz kuwa ni "upuuzi," akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ndiyo mmiliki na mtawala halisi wa lango hilo.
Katika ujumbe aliotuma jana Jumamosi katika mtandao wa kijamii, Mohseni-Eje’i alisema: "Maneno ya kipuuzi na ya uongo ya rais mtenda jinai wa Marekani kuhusu Lango la Hormuz yanatokana na mawazo potofu ya mtu huyo mwenye akili finyu."
"Mmiliki na mtawala wa njia hiyo muhimu ya maji ya kimataifa ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesema Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran.
Eje'i ameeleza haya baada ya Donald Trump kusema kuwa: Baada ya kumaliza kuishinda Iran ambayo inashindwa vibaya sana – hivi karibuni nitatangaza Mlango-Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani, mwisho wa kunukuu.
Mohseni-Eje’i ameeleza kuwa Iran imethibitisha katika nyanja ya kijeshi kuwa Lango-Bahari la Hormuz ni sehemu isiyotenganishika ya himaya na mipaka yake, na inaonya kuwa hatua yoyote ya kichokozi katika njia hiyo muhimu ya majini itasababisha maangamizi na kushindwa upande wowote chokozi.
"Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa na pia kanuni zinazosimamia mamlaka ya kujitawala ya nchi mbalimbali, ukweli kwamba Lango-Bahari la Hormuz ni mali ya Iran ni jambo lililo wazi na lililowekwa bayana," ameongeza Mohseni-Eje’i.
Wakati huo huo afisa wa ngazi ya juu wa ikulu ya Rais wa Marekani (White House) amesema Rais Donald Trump alikuwa anatania wakati alipotamka kwamba ana mpango wa kutangaza Lango Bahari la Hormuz kuwa ni eneo la Marekani.