Majeshi ya Iran yaapa kutorudi nyuma hadi Marekani na Israel zitaposhindwa kikamilifu
Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeapa kutorudi nyuma hata kidogo hadi pale haki za kisheria za nchi zitakapopatikana kikamilifu na wavamizi, yaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, watakapokabiliwa na kipigo cha kukomesha katika eneo hili.
Msimamo huu umetolewa katika taarifa ya Jumapili, ikiadhimisha kumbukumbu ya kurejea kwa mateka wa vita (POWs) wa Iran, ambao walishikiliwa mateka wakati wa vita vilivyolazimishwa dhidi ya nchi hii katika miaka ya 1980 na Saddam, dikteta wa zamani wa Iraq,
Taarifa hiyo imesema: “Kwa irada ya chuma, pamoja na azma thabiti ya wananchi wavumilivu na wastahimilivu wa Iran, Kamandi Kuu ya Majeshi inawahakikishia kuwa haitarudi nyuma kutoka kwa matakwa ya kisheria ya taifa hili na Kiongozi mpendwa wa Jamhuri ya Kiislamu katika kuwakabili wavamizi wa Marekani, hadi hapo maadui wa Kimarekani-Kizayuni watakaposhindwa kabisa katika eneo hili, haki za taifa shujaa la Iran zilindwe, na adui kulazimishwa kusalimu amri.”
Kwa kuungwa mkono na madola makubwa ya Magharibi na ya kikanda, Saddam Hussein alianzisha uvamizi mkubwa mwaka 1980 kwa lengo la kuiteka jimbo la Khuzestan lenye utajiri wa rasilimali nchini Iran, chini ya miaka miwili baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Wairani walishikamana chini ya uongozi wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Khomeini, na kuingia katika medani za vita ili kuwasukuma nyuma wanajeshi wa Iraq na kukomboa maeneo yaliyotekwa.
Vita hivyo vya kutisha vilimalizika mwaka 1988 kwa makubaliano ya usitishaji vita, ambapo dikteta wa Iraq alishindwa kufikia lengo lolote kati ya malengo yake na Iran haikutoa hata inchi moja ya ardhi yake.
Mnamo Agosti 17, 1990, utawala wa Iraq ulilazimika kuanza mchakato wa kuachiliwa kwa mateka na wafungwa wa vita wa Iran kufuatia makubaliano ya kubadilishana mateka yaliyofikiwa mapema mwaka huo.