Kamanda wa IRGC aonya: Adui ajiandae na "mshtukizo wa kimkakati" wa mashambulizi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140734-kamanda_wa_irgc_aonya_adui_ajiandae_na_mshtukizo_wa_kimkakati_wa_mashambulizi_ya_iran
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kwamba, japokuwa hatua za kijeshi za Iran hadi sasa zimebaki kuwa za kujihami tu tangu ulipoanzishwa uadui wa kijeshi dhidi ya taifa hili, lakini vikosi vya jeshi vimejiandaa kikamilifu kuchukua hatua ya kushambulia endapo italazimu, huku akiwaonya maadui kutarajia "mshtukizo wa kimkakati."
(last modified 2026-09-05T16:25:28+00:00 )
Aug 17, 2026 06:10 UTC
  • Kamanda wa IRGC aonya:  Adui ajiandae na

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kwamba, japokuwa hatua za kijeshi za Iran hadi sasa zimebaki kuwa za kujihami tu tangu ulipoanzishwa uadui wa kijeshi dhidi ya taifa hili, lakini vikosi vya jeshi vimejiandaa kikamilifu kuchukua hatua ya kushambulia endapo italazimu, huku akiwaonya maadui kutarajia "mshtukizo wa kimkakati."

Brigedia Jenerali Yadollah Javani, Mkuu wa Masuala ya Kisiasa wa IRGC, ametoa indhari hiyo katika mahojiano na televisheni ya hapa nchini.

Amesisitiza kuwa adui ndiye aliyeanzisha mzozo huo na kubainisha kwamba, majibu ya Iran hadi sasa yamekuwa ya kujihami tu; lakini akaonya kwamba msimamo huu wa kujihami uko tayari kubadilika, kuashiria mabadiliko makubwa na ya kimageuzi katika doktrini ya kimkakati ya jeshi la Iran.

"Adui anapaswa ajue kwamba hawezi kutushtukiza," ameeleza Jenerali Javani na kuongezea kwa kusema: "Badala yake, ni yeye adui ambaye lazima atarajie mshtukizo wa kimkakati."

Ameashiria dikrii za hivi karibuni zilizotoelewa na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran za uteuzi wa makamanda wakuu wa IRGC, akitilia mkazo zaidi mamlaka aliyopewa Kamanda Mkuu mpya, Meja Jenerali Ahmad Vahidi na kubainisha kuwa, dikrii hizo mpya zilizotolewa si mabadiliko ya kiuendeshaji tu bali ni ishara ya wazi kwa maadui kwamba doktrini ya kijeshi ya Iran inabadilika ili kuweza kukabiliana na hata kuzivuka changamoto za vita vya kisasa.

Kwa mujibu wa Jenerali Javani, dikrii iliyotolewa kwa Jenerali Vahidi inatilia mkazo "uhofishaji wa hujuma ya adui kwa kiwango cha juu kabisa" na kuanzisha mbinu mpya ya kiutendaji; na kwamba kuanzia sasa, hatua yoyote ya kujilinda inayochukuliwa na vikosi vya jeshi itachukua sura ya ushambuliaji ili kuzima vitisho kivitendo.../