Vita vya Kiuchumi vya Trump Dhidi ya Iran: Chombo Ambacho Hakifanyi Kazi Tena
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140922-vita_vya_kiuchumi_vya_trump_dhidi_ya_iran_chombo_ambacho_hakifanyi_kazi_tena
Katika kujibu vitisho vipya vya Donald Trump dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, "kung'ang'ania sera zilizofeli kutapelekea tu kushindwa zaidi na kuchochea chuki ya wananchi wa Iran dhidi ya watawala wa Marekani."
(last modified 2026-08-24T10:59:43+00:00 )
Aug 24, 2026 10:58 UTC
  • Vita vya Kiuchumi vya Trump Dhidi ya Iran: Chombo Ambacho Hakifanyi Kazi Tena

Katika kujibu vitisho vipya vya Donald Trump dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, "kung'ang'ania sera zilizofeli kutapelekea tu kushindwa zaidi na kuchochea chuki ya wananchi wa Iran dhidi ya watawala wa Marekani."

Kauli hii ya Abbas Araghchi inaashiria udhaifu wa kimsingi wa mkakati mpya wa Washington. Marekani inataka kufikia matokeo ya kisiasa kwa kutumia njia za kiuchumi, lengo ambalo miongo kadhaa ya mashinikizo ya kiuchumi na kijeshi imeshindwa kulitimiza. Sasa Trump anazungumzia "operesheni kali zaidi ya kiuchumi" dhidi ya Iran na hata kutishia kuziadhibu nchi zinazofanya biashara na Tehran. Jambo la msingi ni kwamba vikwazo si chombo kigeni tena kwa Iran.

Katika miongo minne iliyopita, Tehran imebuni mbinu za kukabiliana na vikwazo, kuelekeza upya biashara, kutafuta washirika mbalimbali wa kiuchumi na kuuza mafuta licha ya vikwazo vilivyopo. Hivyo, suala la msingi leo si ukubwa wa mashinikizo ya Marekani, bali ni uwezo wa Washington wa kubadilisha mashinikizo hayo ya kiuchumi kuwa hatua ya kuilazimisha Iran isalimu amri kisiasa.

Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS) kilisema huko nyuma kwamba, ingawa kampeni ya "mashinikizo ya kiwango cha juu" imeathiri vibaya uchumi wa Iran, lakini imeshindwa kubadili msimamo wa kimkakati wa Tehran. Hata katika suala la mafuta, jitihada za Marekani za kusimamisha kabisa na kufikisha mauzo ya nje ya Iran kwenye kiwango cha sifuri zimekumbwa na vikwazo vikubwa ambapo sehemu kubwa ya mafuta yanayouzwa nje na Iran bado yanaendelea kufika katika masoko ya kimataifa. Ni katika muktadha huu ndipo onyo la Araghchi linapopata uzito na umuhimu mkubwa. Vikwazo huwa na nguvu na kuwa athirifu pale nchi inayolengwa inapokuwa haina njia mbadala na kuwepo muungano mpana unaodhamni utekelezaji wake. La sivyo, kadiri mashinikizo ya kiuchumi ya upande mmoja yanavyoongezeka, ndivyo azma ya nchi iliyowekewa vikwazo inavyoongezeka kwa ajili ya kukabiliana navyo kupitia njia mbadala. Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa pia kimeonya kwamba matumizi ya kupita kiasi na ya upande mmoja ya Washington kuhusu vikwazo, kwa muda mrefu, yatazisukuma nchi kupunguza utegemezi wao kwenye mfumo wa kifedha unaotawaliwa na dola.

Tishio jipya la Trump ni la kushangaza zaidi kuhusu suala hili. Washington inataka kuongeza gharama za kiuchumi za muqawama wa Iran, lakini mashinikizo hayo yanatolewa katika hali ambayo uchumi wa Marekani yenyewe, wenye deni la zaidi ya dola trilioni 40 (kama asilimia 124 ya Pato la Taifa) unakabiliwa na changamoto chungu nzima. Nchi hiyo inakabiliwa na gharama za riba za kila mwaka zinazokaribia dola trilioni 1 na kiwango cha mfumuko wa bei cha takriban asilimia 3.4. Takwimu rasmi za Wizara ya Fedha ya Marekani hufuatilia deni hilo kila siku, ambapo malipo ya riba sasa yamekuwa mojawapo ya masuala muhimu zaidi ya matumizi ya serikali, huku yakizidi hata bajeti ya ulinzi.

Kwa upande mwingine, kubadilisha vikwazo vya kiuchumi kuwa mzingiro wa majini kunapandisha kiwango cha hatari na kulifanya lisiwe suala la nchi mbili pekee. Lango-Bahari la Hormuz si suala linalohusu Iran na Marekani pekee; ni njia muhimu sana ya uchumi wa nishati duniani. Usumbufu wowote wa muda mrefu katika njia hii unaweza kuathiri vibaya bei za mafuta, gharama za bima na usafirishaji, pamoja na viwango vya mfumuko wa bei katika nchi zinazoagiza nishati. Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kupungua kwa kasi kwa idadi ya meli za mafuta zinazopita katika lango la wa Hormuz kumesababisha kupanda kwa gharama za bima na bei za nishati, jambo linaloliweka soko la dunia katika hatari ya kukumbwa na mshtuko mpya.

Katika mazingira haya, vita vya kiuchumi vinaweza kubadilika kutoka kuwa zana ya kuishinikiza Iran na kuwa chanzo cha mashinikizo dhidi ya Marekani na washirika wake. Uchambuzi wa CSIS kuhusu hali ya mambo katika Lango-Bahari la Hormuz unasisitiza kuwa mzozo wa sasa si suala la ushindani wa kijeshi pekee, bali ni jaribio la uwezo wa pande zote mbili katika kuhimili gharama na nguvu zao za majadiliano. Ingawa Washington ina uwezo mkubwa wa kijeshi, lakini ni wazi kuwa hali hiyo haiipi kinga dhidi ya athari za kiuchumi na kisiasa. Kwa hivyo, majibu ya Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lazima yaeleweke katika muktadha wa pambano kubwa zaidi la kisiasa. Marekani inaweza kuweka vikwazo zaidi, kufunga njia za kifedha na kuongeza mashinikizo kwa washirika wa kiuchumi wa Iran, lakini hakuna hata moja ya hatua hizi inayotoa dhamana kuwa mashinikizo ya kiuchumi yatapelekea Iran kusalimu amri kisiasa. Uzoefu wa miongo minne iliyopita unaonyesha kuwa vitisho vya kijeshi na kiuchumi havibadilishi mahesabu ya kiusalama na kisiasa ya Tehran.

Hapa ndipo palipo na dosari katika mkakati wa Trump: ikiwa Washington itafuata tena njia ya vikwazo kwa dhana kwamba nia ya Iran itabadilika kwa maslahi yake, itakuwa inaota tu kwa sababu, badala ya kujaribu kuilazimisha Tehran ilegeze msimamo, itakuwa inahatarisha kusambaza gharama za kiuchumi za mzozo huo ndani ya Marekani yenyewe na kwa uchumi wa dunia. Ujumbe wa Araghchi, kwa kweli ni onyo kuhusu mahesabu hayo ya kimakosa. Sera hiyo ambayo tayari imefanyiwa majaribio mengi huko nyuma na hatimaye kushindwa kufikia malengo yake ya kisiasa mara hii pia hatifanikiwa, hata kama itafuatiliwa kwa vitisho na nguvu zaidi.