Je, vita vipya vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran vitafikia malengo yake?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141048-je_vita_vipya_vya_kiuchumi_vya_marekani_dhidi_ya_iran_vitafikia_malengo_yake
Huku vita vinavyoendeshwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran vikiwa vimekwama na kampeni ya kijeshi kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa, Washington imebadilisha mkakati wake na kuhamisha mwelekeo wa makabiliano kutoka uwanja wa vita vya kijeshi hadi kwenye uwanja wa kiuchumi.
(last modified 2026-08-29T06:45:17+00:00 )
Aug 29, 2026 06:41 UTC
  • Je, vita vipya vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran vitafikia malengo yake?

Huku vita vinavyoendeshwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran vikiwa vimekwama na kampeni ya kijeshi kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa, Washington imebadilisha mkakati wake na kuhamisha mwelekeo wa makabiliano kutoka uwanja wa vita vya kijeshi hadi kwenye uwanja wa kiuchumi.

Kufuatia kushindwa kijeshi Marekani dhidi ya Iran, Scott Bessent Waziri wa Fedha wa Marekani, alitangaza siku ya Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari "Operesheni ya Kutenga Kiuchumi" (Operation Economic Outcast), akitekeleza maagizo ya moja kwa moja ya Trump. Alitangaza kuanzishwa kwa operesheni hiyo inayolenga "kuibana kiuchumi" Iran na kukata njia zake zote muhimu za kifedha. Bassent alifananisha hatua hiyo na "siku ya mashambulizi makubwa ya kiuchumi", hatua kubwa zaidi ya mashambulizi ya kifedha kuwahi kutekelezwa dhidi ya adui, na kuonya kuwa nchi yoyote itakayofanya biashara na Iran "itajumuishwa na Iran katika kutengwa," huku akisisitiza kuwa "hakuna anayeweza kukwepa vikwazo vya Marekani." Alizionya nchi zote duniani, ikiwemo China kwamba, vikwazo vya ziada vitawekwa dhidi ya taasisi yoyote itakayowezesha miamala ya mafuta ya Iran, na kwamba hakuna yeyote atakayesalimika na adhabu ya Washington iwapo hatatii maagizo yake.

Vikwazo hivi vipya vinalenga sekta tano muhimu, rasilimali za kidijitali, teknolojia, dhahabu, usafiri wa anga na usafiri wa baharini, na pia vinajumuisha zaidi ya taasisi, watu binafsi na mashirika 60 ya meli kote duniani. Utawala wa Trump pia umeonya kuwa hatua yoyote ya kuwezesha utakasishaji wa fedha unaoinufaisha Iran itapelekea kufukuzwa wahusika katika mfumo wa kifedha unaotumia dola.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayoukabili mkakati huu mpya wa Washington ni kupungua kwa kiasi kikubwa kwa uungwaji mkono wa umma wa Marekani kwa mzozo unaoendelea na Iran. Kwa mujibu wa utafiti uliotangazwa Jumatatu na Reuters/Ipsos, ni asilimia 31 tu ya Wamarekani ndio wanaunga mkono hatua ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran, kiwango ambacho kimeshuka kutoka asilimia 37 mwezi Machi na asilimia 34 mapema mwezi huu.

Kupungua huku kunatokana hasa na kupungua kwa uungaji mkono miongoni mwa Warepublican, huku kiwango cha kuungwa mkono vita hivyo kikishuka kutoka asilimia 77 mwezi Machi hadi asilimia 69. Wakati huo huo, kiwango cha kukubalika Trump kimefikia kiwango cha chini zaidi tangu aingie madarakani, huku asilimia 33 pekee ya waliohojiwa wakiunga mkono utendaji wake. Aidha, asilimia 83 ya Wamarekani wanaamini kuwa vita hivi itaendelea kwa muda mrefu. Takwimu hizi zinaashiria si tu kupungua kwa uungwaji mkono wa umma kwa vita, bali pia changamoto kwa White House kuhusiana na uhalali wa ndani wa sera zake.

Kwa upande mwingine, ikitumia uzoefu wa karibu miongo mitano katika kukabiliana na vikwazo vya Marekani, Iran imetumia mikakati mbalimbali inayozingatia uelewa wa kina wa nguvu na udhaifu wake yenyewe. Katika taarifa yake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetaja uchumi kuwa "uwanja mkuu wa vita" katika makabiliano na adui, huku likisisitiza umuhimu wa uratibu miongoni mwa taasisi zote zinazohusika na masuala ya uchumi, biashara, mafuta, viwanda, kilimo, benki, na diplomasia ili kudhibiti taathira za vikwazo. Wakati huo huo, Mohammad Mokhber, mshauri na msaidizi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametangaza kuwa Iran imebuni "mkakati wa kukabiliana na hali hiyo" ili kupambana na hatua zote za uhasama wa Marekani, yakiwemo mashinikizo ya kiuchumi.

Turufu muhimu ya Iran katika kukabiliana na mzingiro wa baharini na vita vya kiuchumi ni nafasi yake ya kipekee ya kijiografia katika Lango-Bahari la Hormuz; nchi hii imefanikiwa kubuni mfumo thabiti wa kudhibiti usafiri katika njia hiyo muhimu ya maji. Aidha, viongozi wa ngazi za juu wa Iran, akiwemo Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, wametoa onyo la wazi kwamba ikiwa vita vya kiuchumi vitaongezeka makali, hakuna mafuta yatakayosafirishwa nje kupitia Lango la Hormuz au hata Ghuba ya Uajemi, hili likiwa ni tishio lenye uwezo wa kusababisha mshtuko usio na mfano wake katika masoko ya nishati duniani. Vilevile, Iran inajitahidi kudumisha usafirishaji wa mafuta na usambazaji wa bidhaa muhimu kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo kupitia "meli za kivuli," usafiri wa nchi kavu na njia nyinginezo mbadala.

Kieneo, Iran pia inatumia mkakati wa "karata ya kikanda" ili kukabiliana na hali hiyo. Kutoa vibali maalum kwa meli za Iraq na kufikia makubaliano na Oman kuhusu njia za usafirishaji wa majini ni mifano ya jitihada za Tehran za kuleta mgawanyiko katika muungano wa nchi zinazoungwa mkono na Marekani na kuzilazimu zichukue msimamo wenye mantiki zaidi. Ingawa vita na mzingiro wa majini vimetoa mashinikizo makubwa kwenye uchumi wa Iran, lakini wataalamu wanaamini kuwa kutokana na historia ndefu ya Iran ya kukabiliana na vikwazo na kumiliki kwake mbinu mbalimbali za kupambana na hali hiyo, mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani hayataangusha uchumi wala kuleta mabadiliko yoyote katika mwenendo wa Tehran.

Wakati huo huo, jambo linalotoa changamoto kubwa kwa Marekani katika mvutano wake na Iran ni utata wa wazi kati ya mkakati mkali wa kiuchumi wa Washington na kupungua kwa uungwaji mkono wa mkakati huo ndani ya Marekani.

Utawala wa Trump umeanzisha mashambulizi makubwa ya kiuchumi dhidi ya Iran baada ya kukwama katika kinamasi cha kijeshi na nchi hii, na hivyo kupoteza pakubwa uungaji mkono wa Wamarekani. Kwa upande mwingine, licha ya kukabiliwa na mashinikizo makubwa ya kiuchumi, Iran inamiliki rasilimali muhimu za kimkakati, kama vile Lango-Bahari la Hormuz na uzoefu uliopatikana kutokana na "Uchumi wa Muqawama," ambapo imepata uwezo mkubwa wa kumsababishia adui hasara kubwa isiyovumilika. Matukio yatakayojitokeza katika wiki na miezi ijayo bila shaka yatakuwa si kipimo tu cha kupima uchumi wa Iran ambao umestahimili mashinikizo ya kiuchumi na vikwazo vya Washington kwa miongo kadhaa, bali pia kipimo cha kutathmini ufanisi wa mkakati wa Marekani wa "kunyonga uchumi," hasa wakati ambapo msingi wa kisiasa wa Donald Trump ndani ya Marekani yenyewe umeanza kuyumbayumba zaidi.