Kushindwa "Mashinikizo ya Kiwango cha Juu Zaidi": Namna Vikwazo vya Marekani Vinavyoidhuru Yenyewe
Ripoti mpya zinaonyesha kuwa sera ya Marekani ya "mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi" haina tena uwezo wa kuilazimisha Iran ibadili mienendo yake, na inaweza hata kudhoofisha uwezo wa Washington yenyewe wa kutumia vikwazo kufikia malengo yake.
Jeffrey Sachs, mchumi wa Marekani, anahoji kuwa kuongeza ukali wa vikwazo hakutaifanya Iran kutengwa kimataifa; bali kutapalekea Marekani yenyewe kutengwa. Kauli hii inaakisi ukweli muhimu wa siasa za kimataifa hii leo ambapo Washington haiwezi tena kulazimisha matakwa yake katika uchumi wa dunia kama ilivyokuwa ikifanya katika miaka ya huko nyuma. Ingawa vikwazo vinasalia kuwa wenzo wa nguvu kwa Marekani, lakini hauna tena taathira ya kuamua matokeo ya mwisho. Machapisho ya Foreign Affairs na The Economist nayo yametoa ripoti zinazoashiria kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimefeli. Jeffrey Sachs, Foreign Affairs na The Economist wamefikia hitimisho moja wakitumia mitazamo mitatu tofauti kwamba, sera ya "mashinikizo ya juu zaidi" dhidi ya Iran hayana tena makali yaliyokuwa nayo huko nyuma. Wanasema licha ya kupoteza makali yake, mashinikizo hayo huenda yakawa na matokeo kinyume na matarajio ya watawala wa Marekani ambapo yanaweza hata kuongeza gharama kwa Marekani yenyewe. Sachs anafafanua suala hili kwa kuzingatia kupungua kwa nguvu ya Marekani ya kulazimisha mambo dhidi ya pande nyingine. Kwa mtazamo wake, Washington haiwezi kuziamrisha nchi kama China, Russia au mataifa mengine yasifanye biashara na Iran. Hili ni jambo muhimu sana. Vikwazo vya ngazi ya pili hufanikiwa tu pale wadau wakuu wa uchumi duniani wanapohofia gharama za kukaidi amri ya Marekani, lakini sasa hali hii imebadilika.
China si mshiriki wa pembeni tena katika mfumo wa vikwazo; ni nguvu kubwa ya kiuchumi. Inanunua sehemu kubwa ya mafuta ya Iran na ina uwezo wa kuchukua hatua za kiuchumi za kukabiliana na mashinikizo ya Marekani. Hivyo, kadiri vikwazo dhidi ya Iran vinavyosababisha mvutano wa moja kwa moja katika uhusiano kati ya Washington na Beijing, ndivyo gharama kwa Marekani inavyozidi kuongezeka. Jarida la The Economist linathibitisha ukweli huu kwa mtazamo tofauti. Linasema mitandao ya kibiashara na kifedha ya Iran imekuwa vigumu kugundulika. Biashara ya Iran na China, Falme za Kiarabu (UAE), na washirika wengine wa kiuchumi haitegemei tu njia ambazo Washington inaweza kuzizuia kirahisi, bali mifumo isiyotumia dola na mitandao ya kifedha inayofanya kazi nje ya udhibiti wa Marekani imeanzishwa. Hatua hii ina ujumbe muhimu wa kimkakati, kwamba vikwazo si amri ya kimataifa inayopaswa kutekelezwa bila kuhojiwa tena; bali ni zana ya mashinikizo inayohitajia ushirikiano wa wengine ili kuzaa matunda. Kadiri idadi ya nchi zisizotaka kubeba gharama za ushirikiano huo inavyoongezeka, ndivyo mafanikio ya vikwazo yanavyopungua. Hata hivyo, suala muhimu zaidi kuliko kipengele cha kiuchumi ni suala la kuaminika Marekani kimkakati. Jarida la Foreign Affairs linabainisha kuwa kampeni ya mashinikizo dhidi ya Iran ambayo imeendelea kwa zaidi ya miongo minne imeibua mgogoro wenye gharama kubwa, ambao umefichua mapungufu ya sera hiyo. Lengo la mashinikizo hayo lilikuwa kuilazimisha Iran ibadilishe mwenendo na kusalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani lakini hilo halijafikiwa.
Ni kweli kwamba Iran inakabiliwa na mashinikizo ya kiuchumi, ukweli ambao hauwezi kukanushwa, na bila shaka vikwazo hivyo vimeisababishia gharama kubwa. Hata hivyo, kuna tofauti muhimu kati ya "madhara ya kiuchumi" na "mabadiliko ya kimkakati." Vikwazo vinaweza kuweka mashinikizo kwenye uchumi wa nchi, lakini si lazima vibadilishe mahesabu yake ya kiusalama na kisiasa. Hapa ndipo hasa sera ya Marekani inapokumbwa na changamoto. Washington inatambua gharama za kuweka mashinikizo lakini inashindwa kuzingatia gharama inazopata kutokana na kukabiliwa na upinzani dhidi ya mashinikizo hayo. Kwa upande mwingine, Iran imejaribu kuhamishia gharama za mashinikizo hayo kwa upande hasimu.
Lango-Bahari la Hormuz lina umuhimu wa kipekee katika mlingano huu. Usumbufu wowote katika njia hii ya maji huathiri moja kwa moja masoko ya nishati na uchumi wa dunia, hivyo, mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Iran yanaweza kugeuka kirahisi kuwa suala la kimataifa. Gazeti la The Economist pia limetoa tahadhari kwamba kurejelewa mashinikizo ya kiuchumi kunaweza kuwa na matokeo kinyume na inavyotarajiwa. Ikiwa Washington inadhani kwamba mashinikizo yanayoongezeka yanaweza kuilazimisha Tehran kurudi nyuma, inaweza kukumbana na taathira zinazoongeza gharama za mashinikizo hayo. Katika hali kama hiyo, vikwazo hubadilika kutoka kuwa chombo cha majadiliano hadi kuwa kichocheo cha kuongezeka mgogoro.
Jarida la Foreign Affairs linaelezea mabadiliko haya kama "mzunguko wenye muelekeo wa upande mmoja." Kila duru ya mashinikizo huisukuma Washington kuelekea hatua ya baadaye ya mashinikizo, lakini bila kufikiwa lengo kuu la mwisho. Matokeo yake ni kuongezeka gharama na kupungua machaguo ya kisiasa, ambao ni mkwamo wa kweli wa kimkakati. Marekani haiwezi kuiteka Iran au kudhamini mabadiliko ya utawala kupitia mashambulizi ya anga, wala haiwezi kutegemea vikwazo pekee kuilazimisha ijisalimishe.
Marekani lazima ilipe gharama za kisiasa na kiuchumi ili kudumisha mashinikizo, huku Iran ikilazimika kubeba gharama ya kiuchumi ili kuhimili mashinikizo hayo. Tofauti muhimu ipatikana katika ukweli kwamba Iran imeishi na vikwazo kwa miaka mingi na bila shaka imejibunia mbinu za kukabiliana navyo; kinyume na Marekani ambayo kadiri inavyotumia vikwazo, ndivyo inavyowasukuma washirika wake kutafuta njia mbadala za kujitetea na kujidhaminia salama na maslahi yao. Hivyo, kufeli kwa mkakati wa "mashinikizo ya juu zaidi" hakumaanishi kuwa vikwazo vimepoteza kabisa taathira zake, bali kunamaanisha kuwa vikwazo pekee haviwezi tena kudhamini matokeo ya kisiasa yanayotarajiwa na Washington. Hii ni tofauti kubwa na ya msingi. Ujumbe wa ripoti hizo tatu uko wazi. Marekani bado ina uwezo wa kuweka vikwazo, lakini si nguvu kuu na ya pekee yenye kuamua mambo kama ilivyokuwa huko nyuma. Iran inaendelea kukabiliwa na mashinikizo, lakini haijatengwa kimataifa. Aidha, China na mataifa mengine yenye nguvu duniani hayako tayari kuoanisha kanuni zao za kiuchumi na matakwa ya Washington bila kuathirika au kupata hasara. Hivyo, iwapo Washington itaendelea kutumia vikwazo badala ya diplomasia, hatimaye itaisukumua dunia ukutani na hivyo kuilazimisha kuunda mfumo huru zaidi usiotegemea Marekani, badala ya kuitenga Iran. Hapa ndipo hasa mkakati wa "mashinikizo ya juu zaidi" unapoleta matokeo yaliyo kinyume na matarajio ya wapangaji na watekelezaji wake.