Iran: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya kisiwa cha Lark ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141106-iran_mashambulizi_ya_marekani_dhidi_ya_kisiwa_cha_lark_ni_ukiukaji_wa_wazi_wa_mkataba_wa_umoja_wa_mataifa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa kuhusu uvamizi wa kijeshi uliofanywa na jeshi la Marekani dhidi ya kisiwa cha Lark, pamoja na jibu la kiulinzi lililotolewa na Iran.
(last modified 2026-08-31T16:56:09+00:00 )
Aug 31, 2026 12:05 UTC
  • Iran: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya kisiwa cha Lark ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa
    Iran: Mashambulizi ya Marekani dhidi ya kisiwa cha Lark ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa kuhusu uvamizi wa kijeshi uliofanywa na jeshi la Marekani dhidi ya kisiwa cha Lark, pamoja na jibu la kiulinzi lililotolewa na Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza katika taarifa yake kwamba, kwa mujibu wa haki ya asili ya kujilinda, majeshi yenye nguvu ya Iran yamezilenga kwa mashambulizi makali ya kujihami kambi za kijeshi za Marekani zilizoko nchini Jordan, ambazo zilitumika kama chanzo na kituo cha kuunga mkono uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran.

Katika taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya kisiwa cha Lark, kusini mwa Iran, ikisema kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa Ibara ya 2, Kifungu cha 4 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Wizara hiyo pia imelikumbusha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wajibu wake wa kuhakikisha upande uliofanya uchokozi unawajibishwa.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inamkumbusha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mwenyekiti wa Baraza la Usalama na serikali zote ambazo zimeeleza wasiwasi wao kuhusu kuendelea hali ya ukosefu wa usalama katika Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Hormuz, kwamba sababu pekee ya kuhatarishwa usalama wa njia za meli katika eneo hilo ni hatua haramu na za kichokozi zinazofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Taarifa hiyo inasema kuwa, hatua hizo zilianza kwa shambulio dhidi ya Iran tarehe 28 Februari mwaka huu na zimeendelea katika kipindi cha miezi sita iliyopita kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuzingirwa kwa njia ya bahari pamoja na hatua nyingine za uchochezi na uingiliaji mambo ya ndani ya taifa hili.

Wakati huo huo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa Kikosi chake cha Anga kimeshambulia maeneo na kambi za kijeshi za Marekani huko Jordan, na kutoa jibu la haraka kwa shambulio la kigaidi la Marekani katika Kisiwa cha Larak nchini Iran jana usiku.