Rais Pezeshkian: Kuna makundi nchini Marekani yanayoona maslahi yao yapo katika kuendelea vita
-
Rais Pezeshkian: Kuna makundi nchini Marekani yanayoona maslahi yao yapo katika kuendelea vita
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna makundi nchini Marekani yanayoona maslahi yao yapo katika kuendelea vita na hivyo yanataka vita viendelee.
Dkt. Masoud Pezeshkian amesema hayo pembezoni mwa Mkutano wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na Shanghai Plus nchini Kazakhstan, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi.
Katika mazungumzo hayo, Pezeshkian ameishukuru New Delhi kwa mshikamano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa hali ya vita hivi karibuni, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kidiplomasia kwa ajili ya kudumisha amani na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Akizungumzia msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu matukio ya kikanda, amesema:
“Tangu mwanzoni mwa uongozi wa serikali yetu, juhudi zetu zimekuwa zikilenga kuhakikisha amani na usalama, pamoja na kutatua masuala kupitia njia ya mazungumzo na majadiliano. Hata hivyo, kwa masikitiko, utawala wa Marekani badala ya kutumia njia za kidiplomasia, umechagua njia ya vita, ukosefu wa usalama na kulazimisha matakwa yake kwa kutumia nguvu na mabavu.
Pezeshkian, akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haikaribishi vita, amebainisha kwamba: “Wajibu wetu unatutaka kuwalinda wananchi dhidi ya hatari na ukosefu wa usalama, na kuweka mazingira yatakayowawezesha kupata amani, utulivu na usalama.”
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa India ameeleza furaha yake ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akisema:
“Katika kipindi hiki kigumu cha hivi karibuni, tulijitahidi kuendeleza na kudumisha ushirikiano na mawasiliano yetu na Iran.”
Narendra Modi, akiashiria uzoefu na mitazamo ya Dkt. Pezeshkian kuhusu amani na usalama, aliongeza:
“Kwa kutambua kwangu shakhsia yako, nimegundua kwamba wewe ni mtu unayependa amani, na ninaamini unaweza kuwa na nafasi muhimu katika njia ya kufanikisha amani. Nina hakika kwamba juhudi zako hatimaye zitazaa matokeo mazuri.”