Pezeshkian: Iran na Russia zinaweza kusimama kidete dhidi ya sera ya upande mmoja ya Marekani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dkt Masoud Pezeshkian, amesema kuwa Marekani haina uhalali wowote wa kisheria wala wa kimataifa wa kuiwekea Iran vikwazo vya kidhalimu, akisisitiza kuwa Tehran na Moscow zinaweza kushirikiana bega kwa bega ili kukabiliana na sera ya upande mmoja (unilateralism) ya Marekani inayovuruga utulivu wa dunia.
Rais Pezeshkian ametoa kauli hiyo siku ya Jumanne wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Shirikisho la Russia, Vladimir Putin, kando ya Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) uliofanyika mjini Bishkek, Kyrgyzstan.
Akimshukuru Rais Putin kwa msimamo thabiti wa Russia katika kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu, Rais Pezeshkian alibainisha kuwa madola makubwa ya kibeberu hayana haki ya kutumia uwezo wao wa kijeshi na kisiasa kufanya uchokozi na uvamizi huku yakikanyaga sheria, kanuni na mikataba ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Iran, Rais Pezeshkian alimweleza mwenzake wa Russia: “Tunathamini sana misimamo yenu imara ya kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Aidha, aliyataja mahusiano baina ya Tehran na Moscow kuwa ni ya kimkakati na yenye mashiko ya kina, akisisitiza kuwa uhusiano huo unapita kiwango cha ushirikiano wa kawaida wa nchi mbili.
Kwa upande wake, Rais Vladimir Putin amebainisha mshikamano wake kamili na wananchi shupavu wa Iran mbele ya mashinikizo na uadui wa Marekani na utawala ghasibu wa Kizayuni, akisisitiza kuwa Moscow itaendeleza na kudumisha ushirikiano wake wa kiuchumi na kibiashara na Tehran bila kujali changamoto za kijeshi na mikwaruzo ya kisiasa inayoendelea.
Kiongozi huyo wa Russia aliongeza kuwa mahusiano kati ya Moscow na Tehran yanaimarika katika nyanja mbalimbali kwa “kasi thabiti na ya kuridhisha,” yakiongozwa na makubaliano ya kina ya ushirikiano yaliyopo baina ya mataifa hayo mawili.
Taarifa rasmi ya Ofisi ya Rais wa Iran imesema: “Katika mkutano huo, tathmini ya kina ilifanyika kuhusu hali ya sasa ya mahusiano baina ya Iran na Russia, na pande zote mbili zilijadili mikakati ya kuimarisha na kupanua wigo wa ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo."
Mkutano huu muhimu umefanyika wakati ambapo Marekani imeendeleza lugha ya vitisho vya kutaka kutoa duru mpya ya vikwazo haramu dhidi ya nchi zinazoendeleza ushirikiano wa kiuchumi na Iran, ikiwemo washirika wake wakuu wa kimkakati, Russia na China.