IRGC yaangamiza askari wengi Wamarekani walioko Jordan baada ya US kuua raia wa Iran kwenye sherehe ya harusi
Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimetekeleza mfululizo wa operesheni kali za kulipiza kisasi ambazo zimehusisha mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani zilizolenga kambi na maslahi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi kufuatia vitendo vya hivi karibuni vya utawala huo wa kigaidi vya kuanzisha uchokozi usio na sababu, ambao umepelekea kuuawa shahidi raia kadhaa wasio na hatia wa Jamhuri ya Kiislamu akiwemo mtoto mdogo.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitoa taarifa usiku wa kuamkia leo kuhusiana na kuanza operesheni hiyo ya kulipiza kisasi likisema: "Operesheni kali za Jeshi la Iran za kukabiliana na adui wa kigaidi Marekani zimeanza dakika chache zilizopita. Kambi na maslahi ya Marekani katika eneo lote sasa yanashambuliwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani za Iran".
Operesheni hizo zinafuatia matukio mengi ya uchokozi usio na sababu dhidi ya maeneo kadhaa ndani ya Jamhuri ya Kiislamu, hususan maeneo ya kusini mwa nchi.
Hujuma za karibuni zaidi za uchokozi huo zimehusisha shambulio lililolenga Kaunti ya Sirik ya mkoa wa kusini mwa Iran wa Hormozgan, ambapo baki la kombora lilipiga jengo la makazi katika mji wa Kouhestak yalipokuwa yakifanyika maandalizi ya sherehe ya harusi.
Hadi sasa, watu watano akiwemo mtoto mmoja wamethibitishwa kuuawa shahidi, na wengine 63 wamejeruhiwa.
Mashambulizi ya awali ya jeshi la kigaidi la Marekani yalilenga Kaunti za Chabahar na Konarak huko Sistan na Baluchestan, mkoa mwingine wa kusini mwa Iran, na Kisiwa cha Larak katika Mlango-Bahari wa Hormuz, na kupelekea vikosi vya ulinzi vya Iran kujibu mapigo kwa kutekeleza operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko Jordan na katika Muungano wa Falme za Kiarabu.
Taarifa ya karibuni ya IRGC imesema, katika operesheni ya kulipiza kisasi, Kikosi cha Anga cha jeshi hilo kimefanya shambulio zito la makombora ya balestiki dhidi ya kambi ya Wanamaji ya Marekani inayojulikana kama Kambi ya Titiin iliyoko ndani ya ardhi ya Jordan kwenye ufukwe wa Ghuba ya Aqaba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shambulio hilo limeua idadi kubwa ya askari wa Marekani na kuharibu vituo kadhaa muhimu vya jeshi hilo la kigaidi pamoja na helikopta zake za mashambulizi.
Taarifa nyingine ya IRGC imesema, shambulio zito la makombora ya balestiki limetekelezwa dhidi ya maegesho yaliyokuwa na ndege zisizo na rubani za masafa marefu aina ya RQ-4 na MQ-9 katika kambi ya anga ya Marekani huko Jordan inayojulikana kama Prince Hassan, ambapo ndege kadhaa zisizo na rubani zimeteketezwa, marubani kadhaa na wafanyakazi wa kiufundi wa ndege wameuawa, na vituo vyao kadhaa vya miundombinu ya kiufundi pia vimeharibiwa…/