Qalibaf: Marekani ‘inaua kama Shetani’: Alaani shambulio dhidi ya sherehe ya harusi kusini mwa Iran
-
Marekani ‘inaua kama Shetani’
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf amelaani shambulio la Marekani dhidi ya sherehe ya harusi kusini mwa Iran, akisema kuwa kulenga raia katika shule, ukumbi wa michezo na sherehe ya harusi kunaonyesha namana Washington inavyotenda na kuua "kama Shetani."
Katika chapisho alilotuma katika akaunti yake kwenye mtandao wa X siku ya Jumatano, Qalibaf amelitaja shambulio hilo la Marekani kuwa sehemu ya mfululizo wa mashambulio ya nchi hiyo dhidi ya raia; akikumbusha mashambulizi ya awali yaliyofanywa na Marekani katika shule ya msingi ya mji wa Minab na katika ukumbi wa michezo mjini Lamerd katika Vita vya Ramadhani.
“Katika Shule ya Minab watoto waliuawa kikatili. Ukumbi wa michezo wa Lamerd- watoto walichinjwa. Kwenye sherehe ya harusi ya Kouhestak- watoto wameuawa pamoja na familia zao,” ameandika Spika wa Bunge la Iran katika akaunti yake ya X leo Jumatano.
“Ikiwa dola linatenda kama shetani, linachagua walengwa kama shetani, na kuua kama shetani, basi hilo ni Shetani. Je, nchi hiyo inamlinda shetani mdogo anayefanya mambo hayo? Basi hiyo ndiyo Shetani Mkubwa.”
Inafaa kuashiria hapa kuwa jeshi la Marekani lilishambulia sherehe ya harusi huko Kouhestak katika Wilaya ya Sirik mkoani Hormozgan nchini Iran majira ya saa mbili usiku jana Jumanne. Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu watano na kujeruhi wengine 68, huku mtoto aliyekuwa na umri miaka minne akiwa miongoni mwa waliouliwa shahidi.