IRGC yapiga makao ya kamandi ya Marekani na eneo la kuegeshea droni huko Kuwait
-
IRGC yashambulia kambi za US nchini Kuwait
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) limesema kuwa vikosi vyake vimeshambulia makao makuu ya kamandi na makazi ya wanajeshi wa Marekani katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Ali Al-Salem nchini Kuwait, na kuteketeza ghala la ndege zisizo na rubani (droni) na eneo la maandalizi ya kurushia ndege hizo. Shambulizi hilo limeharibu idadi kadhaa ya ndege zisizo na rubani za jeshi la kigaidi la Marekani.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano Idara ya Uhusiano wa Umma ya IRGC imesema kuwa operesheni hiyo ilifanywa kujibu shambulio la Marekani dhidi ya raia nchini Iran.
Taarifa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imeongeza kuwa hatua hiyo ya kulipiza kisasi imechukuliwa baada ya vikosi vya jeshi la Marekani kubadilisha sherehe ya harusi ya wanandoa vijana wa Kisuni huko Sirik, kusini mwa Iran, kuwa maombolezo kwa kushambulia nyumba ya makazi ya raia.
Karibu raia 70 wamejeruhiwa katika shambulio hilo, huku watu watano, akiwemo mtoto mmoja, wakiuawa.
"Kufuatia uhalifu huo, alfajiri ya leo, wapiganaji shupavu wa Kikosi cha Nchi Kavu cha IRGC sambamba na kushambulia kambi za Marekani katika nchi za Jordan, Bahrain na Erbil kaskazini mwa Iraq wamefanya shambulio la pamoja la makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kamandi Kuu na makazi ya wanajeshi wa Marekani katika kambi ya Ali Al-Salem," imeeleza taarifa ya IRGC.
IRGC imesema kuwa shambulio hilo limeua idadi kadhaa ya wanajeshi wa Marekani na limefuatiwa na mashambulizi kadhaa dhidi ya ghala la ndege zisizo na rubani pamoja na eneo la kurushia ndege hizo lililotumika katika mashambulizi dhidi ya Iran. Imesema kuwa ndege kadhaa zisizo na rubani ziliharibiwa na ghala hilo likateketea kwa moto.