Baada ya shambulio harusini; IRGC yasema: Viongozi wa US wanapasa kuwajibishwa kwa jinai za kivita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141180-baada_ya_shambulio_harusini_irgc_yasema_viongozi_wa_us_wanapasa_kuwajibishwa_kwa_jinai_za_kivita
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetangaza kuwa Washington lazima iwajibishwe kwa jinai za kivita zilizofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani katika Mkoa wa Hormozgan kufuatia shambulio la anga lililolenga sherehe ya harusi.
(last modified 2026-09-03T12:21:49+00:00 )
Sep 03, 2026 10:17 UTC
  • Jeshi la IRGC
    Jeshi la IRGC

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetangaza kuwa Washington lazima iwajibishwe kwa jinai za kivita zilizofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani katika Mkoa wa Hormozgan kufuatia shambulio la anga lililolenga sherehe ya harusi.

Taarifa IRGC iliyotolewa leo Alhamisi imeeleza kuwa shambulio la anga la Marekani katika eneo la Kouhestak, mkoani Hormozgan ni jinai ya kivita iliyouwa na kujeruhi watu takriban 70. Makumi ya watu wameuawa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya anga ya Marekani.  

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran limeeleza kuwa kitendo hicho cha uchokozi ni sehemu ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya mikusanyiko ya raia wa kawaida, ikitolea mfano mashambulizi ya huko nyuma yaliyolenga sherehe za harusi nchini Afghanistan, Iraq na Yemen.

Taarifa ya IRGC imeongeza kuwa viongozi wa Marekani badala ya kuomba radhi, kwa mara nyingine tena wameibua madai ya uwongo na kukwepa kuwajibika, sawa na walivyofanya huko Minab, Lamerd na Qeshm hapa nchini.

Jeshi la IRGC limesisitiza kuwa viongozi wa Marekani lazima wawajibishwe na limeitaka Washington ieleze hatua zake kwa jamii ya kimataifa.

"Marekani imeshindwa kutimiza malengo yake katika vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran, na tunaionya kwamba uchokozi wake unaoendelea dhidi ya raia hautasalia bila jibu," imeeleza taarifa ya IRGC.

Jioni ya Jumanne, jeshi la Marekani lilishambulia kinyama sherehe ya harusi katika Bandari ya Kouhestak, katika Wilaya ya Sirik kusini mwa Iran. Makumi ya watu waliuawa shahidi na kujeruhiwa; huku wanawake na watoto wakiwa miongoni mwa wahanga.