Meja Jenerali Vahidi: Damu isiyo na hatia ya mashahidi madhulumu wa Kohestak haitapotea
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141188-meja_jenerali_vahidi_damu_isiyo_na_hatia_ya_mashahidi_madhulumu_wa_kohestak_haitapotea
Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe maalumu na kusema kuwa: Damu isiyo na hatia ya mashahidi waliouliwa kidhulma na magaidi wa Kimarekani huko Kohestak haitapotea kamwe na wahusika wakiwemo makamanda waliofanya jinai hiyo ya kivita wataburuzwa mahakamani.
(last modified 2026-09-04T03:21:46+00:00 )
Sep 04, 2026 03:20 UTC
  • Meja Jenerali Vahidi: Damu isiyo na hatia ya mashahidi madhulumu wa Kohestak haitapotea

Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe maalumu na kusema kuwa: Damu isiyo na hatia ya mashahidi waliouliwa kidhulma na magaidi wa Kimarekani huko Kohestak haitapotea kamwe na wahusika wakiwemo makamanda waliofanya jinai hiyo ya kivita wataburuzwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Meja Jenerali Ahmad Vahidi, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kulaani shambulio la anga lililofanywa na vikosi vya kigaidi vya Marekani kwenye sherehe ya harusi katika eneo la Kohestak la Kaunti ya Sirik, Mkoa wa Hormozgan kusini mwa Iran na kuua shahidi na kujeruhiwa makumi ya raia wasio na hatia, amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitoacha damu ya raia hao madhulumu ipotee bure.

Katika ujumbe wake huo Meja Jenerali Vahidi amezungumzia ukubwa wa jinai hiyo na kusema kuwa ni ugaidi usio na chembe ya ubinadamu uliofanywa na watawala magaidi wa Marekani, ambao lengo lao ni "kuondoa furaha katika maisha ya taifa tukufu la Iran na kusababisha hofu na ugaidi miongoni mwa raia wake wasio na hatia."

Meja Jenerali Vahidi amesisitiza kwamba Iran itachukua hatua dhidi ya wahusika na makamanda wa jinai hiyo ya kivita na kwamba Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na majeshi mengine ya Jamhuri ya Kiislamu yataendelea kutekeleza vizuri majukumu yao ya kudumisha usalama na utulivu wa nchi.

Inafaa kukumbusha hapa kwamba katika shambulio la kigaidi lililofanywa na Marekani dhidi ya sherehe za harusi kwenye nyumba moja ya mji wa bandari wa Kohestak kusini mwa Iran, raia watano waliuawa shahidi kikiwemo kitoto kidogo cha miaka minee na zaidi ya raia wengine 70 walijeruhiwa.