Qatar imethibitisha kuwa mashambulio ya Iran ndani ya ardhi ya nchi hiyo yalilenga vituo vya kijeshi tu vya Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ameashiria hati rasmi ya Qatar iliyowasilishwa kwa Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) ikithibitisha kwamba operesheni halali za kujihami za Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko katika ardhi ya Qatar zilielekezwa kwenye vituo vya kijeshi tu vya Marekani.
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa X, Baghaei amenukuu mchango wa Qatar katika kikao cha dharura cha Baraza la ITU, ikieleza kwamba mashambulizi ya Iran "yalielekezwa kwenye vituo vya kijeshi vya Marekani. […] Hakuna maeneo ya raia yaliyolengwa."
Hati hiyo, iliyoandaliwa kama tathmini ya hatari ya kihadhari na ya usalama, ilibainisha kuwa "karibu mashambulizi yote yalielekezwa kwenye vituo vya kijeshi vya Marekani, isipokuwa shambulio moja dhidi ya vituo vya gesi huko Ras Laffan mnamo tarehe 18 Machi."
Iliongeza kuwa hakuna maeneo ya raia yaliyolengwa na kutathmini hatari ya sasa kwa usalama wa Qatar kutokana na shughuli zinazoendelea kuwa ni ndogo.
Baghaei amesema, kesi pekee iliyoashiriwa na Qatar ilihusisha vituo vilivyokuwa vinahudumia na kusaidia uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran. "Hata hivyo, ikumbukwe kwamba vituo vilivyopigwa siku hiyo vilikuwa vinahudumia uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran," amekumbusha msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Aidha, ameonyesha tofauti kubwa iliyopo kati ya utaratibu wa Iran na mtindo wa muda mrefu wa Washington wa kufanya mashambulio ya kiholela.
"Hii inakinzana kikamilifu na rekodi ndefu ya Marekani ya mashambulizi ya makusudi dhidi ya maeneo ya kiraia ya skuli, hospitali, sehemu za makazi, sherehe za harusi, madaraja, na mengineyo," amebainisha Baghaei.
Ameongeza kuwa kuna "tofauti kubwa kati ya taifa lililostaarabika ambalo limejifunza umuhimu wa kuzingatia kanuni za maadili na kibinadamu hata katika hali na mazingira magumu kabisa, na watawala wanaoshupalia vita ambao hawazingatii utawala wa sheria au maadili katika makadirio ya nguvu zao za kimadaraka."
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeeleza bayana, tena mara kadhaa kwamba operesheni zake za kijeshi katika ardhi za nchi za eneo zinalenga vituo vya kijeshi tu vya utawala wa kigaidi wa Marekani na wala si tishio kwa nchi hizo jirani au raia wao…/