Marekani Yakata Tamaa Kimkakati: Kuanzia Kushindwa Kijeshi hadi Vita vya Kiuchumi Dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141216-marekani_yakata_tamaa_kimkakati_kuanzia_kushindwa_kijeshi_hadi_vita_vya_kiuchumi_dhidi_ya_iran
Katika onyesho jingine la ubabe na upuuzaji wa sheria za kimataifa, Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani amezitishia nchi huru kuhusu ushirikiano wao na Iran, akisema kwamba hakuna mtu yeyote anayepaswa kuiunga mkono Tehran.
(last modified 2026-09-05T07:17:03+00:00 )
Sep 05, 2026 07:03 UTC
  • Marekani Yakata Tamaa Kimkakati: Kuanzia Kushindwa Kijeshi hadi Vita vya Kiuchumi Dhidi ya Iran

Katika onyesho jingine la ubabe na upuuzaji wa sheria za kimataifa, Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani amezitishia nchi huru kuhusu ushirikiano wao na Iran, akisema kwamba hakuna mtu yeyote anayepaswa kuiunga mkono Tehran.

Akizungumza na Fox News mnamo Septemba 2 kuhusu vikwazo dhidi ya Iran, Bessent alitangaza kwamba ujumbe wake kwa kila mtu ni kujitenga na Iran na kwamba hakuna mtu anayepaswa kuiunga mkono nchi hii. Alisema vikwazo vinaweza kujumuisha "mashirika ya ndege, makampuni ya meli na mali za kidijitali." Hatua ya hivi karibuni ya Marekani kuongeza makali ya vita vya kiuchumi dhidi ya Iran, ikijumuisha lugha ya vitisho ya Scott Bessent dhidi ya upande wowote utakaoshirikiana na Tehran, si tu kwamba inaakisi kina cha hali ya kukata tamaa kimkakati inayoikabili Washington, bali pia inatokana na kufeli kwake vibaya katika makabiliano ya kijeshi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mpango huo ulioanzishwa chini ya kaulimbiu ya "Operesheni ya Kuitenga Iran Kiuchumi," ukiwa na lengo la "kuibana Iran kiuchumi", kwa hakika ni jaribio la kufidia mapungufu na pia kujaribu kufikia malengo ambayo mashinikizo ya kijeshi yameshindwa kuyadhamini.

Upuuzaji wa China na Russia pamoja na mataifa mengine yanayoshindana na nchi za Magharibi, kuhusu vikwazo na vitisho hivyo vya Marekani, unatokana na mahesabu yao ya kina ya kijiopolitiki na kiuchumi ambayo yako nje ya uwezo wa Washington. Kauli za hivi karibuni za viongozi wa Iran zinathibitisha kuwa si China na Russia pekee ndizo zinapinga ubabe huo wa Marekani, bali mataifa mengine pia yanatarajiwa kupinga mashinikizo hayo ya kiuchumi ya Washington. Msimamo huu bila shaka unatoa changamoto kubwa kwa mkakati wa Washington wa kutaka kuitenga Iran kiuchumi.

Sababu kuu inayoiwezesha China kuhimili mashinikizo ya Marekani ni maslahi yake muhimu ya kiuchumi. Beijing imeonyesha wazi kuwa, iwapo maslahi yake ya kiuchumi yatahatarishwa na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani, itayapigania maslahi hayo kwa nguvu zake zote. Ukweli huu unathibishwa na hatua ya China ya kununua zaidi ya asilimia 80 ya mauzo ya nje ya mafuta ya Iran mwaka 2025 na kupokea takriban mapipa milioni 1.2 kwa siku mwaka huu, kiwango ambacho ni cha chini kidogo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Utegemezi huu wa kiuchumi unawakilisha mstari mwekundu ambao Beijing haitaruhusu Washington kuuvuka. Mbali na hayo, muundo wa viwanda vya kusafisha mafuta vya China vinavyojulikana kama "teapot refineries", ambavyo kimsingi ni vituo huru vya sekta binafsi vyenye utegemezi mdogo kwa mfumo wa kifedha wa Marekani, umeandaa njia madhubuti ya kukwepa vikwazo, na hivyo kuifanya Washington ushindwe kutoa mashinikizo athirifu dhidi ya taasisi hizo. Viwanda hivi vya China ndio wanunuzi wakubwa zaidi wa mafuta ya Iran yaliyowekewa vikwazo.

Kwa upande mwingine, Russia, kutokana na sababu za kimkakati na kimfumo, haioni kuwa inalazimika kufuata maagizo ya Marekani. Kwa kuwa imekuwa ikilengwa kwa muda mrefu na vikwazo vikali vya Washington, Moscow inafanya shughuli zake nje ya mfumo wa kiuchumi unaoongozwa na Marekani, hali ambayo inafanya taathira za mashinikizo ya Washington dhidi ya nchi hiyo kutokuwa na tija. Mkataba wa kimkakati wa miaka 20 uliotiwa saini kati ya Russia na Iran, pamoja na ushirikiano wao mpana wa kijeshi na kiuchumi, unaashiria azma thabiti ya Kremlin ya kuimarisha "Mhimili wa Muqawama" dhidi ya utawala wa kimabavu wa Marekani. Moscow imeeleza waziwazi hatua hizi kuwa ni "mashinikizo yasiyo ya kisheria" na imepinga matumizi ya vikwazo kama njia ya kuzilazimisha nchi nyingine kutekeleza matakwa ya upande mmoja. Kudiriki kupuuzwa kwa vikwazo hivi haukuwezekani bila kuzingatia muktadha uliosababisha hali hiyo, yaani, kufeli kwa mkakati wa Marekani katika kampeni yake ya kijeshi dhidi ya Iran. Baada ya miezi kadhaa ya vita na gharama kubwa za kifedha na roho za watu, Washington imehitimisha kuwa chaguo la kijeshi si tu limeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa, bali pia limesababisha madhara makubwa kwa uchumi wa Marekani na hadhi yake kimataifa. Hatua ya kuelekea kwenye vita kamili vya kiuchumi kimsingi ni kukiri kimyakimya kushindwa kwa nguvu za kijeshi, na ni jaribio la kufanikisha kile ambacho kimeshindikana katika uwanja wa vita. Lugha inayotumika ya eti "kunyonga uchumi" na "kutengwa kabisa" Iran, inaashiria hali ya kukata tamaa na kupoteza imani kuhusu mbinu za kijeshi, badala ya kuwa inaonyesha nguvu.

Wakati huo huo, vita vipya vya kiuchumi vya Marekani vinakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kimuundo vinavyotia shaka kubwa kuhusu uwezekano wa kufikia malengo yake. Marekani sio tena utawala pekee unaoongoza duniani kiuchumi kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, na majaribio ya kuweka vikwazo vya upande mmoja na vya daraja la pili katika hali ya sasa yana hatari kubwa. Vikwazo vyovyote vipya dhidi ya vyombo vya China vinaongeza hatari ya mgogoro mpana wa kiuchumi kati ya Marekani na China, hatari ambayo Washington haiko tayari kuikabili. Ni wazi kuwa hatua za hivi karibuni za Marekani dhidi ya Iran haziashirii nguvu, bali zinaakisi kupungua kwa udhibiti wake kimataifa na kushindwa kwake kimkakati katika kukabiliana na Iran. Upuuzaji wa vikwazo vya Marekani unaoonyeshwa na mataifa kama vile China na Russia dhidi ya vitisho vya kimabavu vya watawala wa Washington unaashiria mabadiliko makubwa katika uwiano wa nguvu duniani na mwisho wa enzi za maamuzi ya upande mmoja ya Marekani. Kwa kutumia vizuri uhalisia huu wa kijiopolitiki na kunufaika na mipasuko iliyojitokeza katika misimamo ya kimataifa dhidi yake, Iran inaweza kuhimili kwa mafanikio vita hivi vya kiuchumi na kudhihirisha tena kwamba hatua za ubabe na vitisho vya kimabavu havitaiwezesha Marekani kufikia malengo yake.