Makamu wa Rais: Iran imezishinda njama za kijeshi, imejiweka tayari kwa vita vya kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141238-makamu_wa_rais_iran_imezishinda_njama_za_kijeshi_imejiweka_tayari_kwa_vita_vya_kiuchumi
Makamu wa Kwanza wa Rais Mohammad Reza Aref amesema Iran imezishinda njama za mtawalia za kijeshi, kiuchumi, kijamii na kisiasa zilizolenga kuipindua Jamhuri ya Kiislamu au kuifanya isalimu amri, na kwamba sasa inajiandaa kukabiliana na awamu mpya ya vita vya kiuchumi.
(last modified 2026-09-06T03:02:31+00:00 )
Sep 06, 2026 03:01 UTC
  • Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Reza Aref
    Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Reza Aref

Makamu wa Kwanza wa Rais Mohammad Reza Aref amesema Iran imezishinda njama za mtawalia za kijeshi, kiuchumi, kijamii na kisiasa zilizolenga kuipindua Jamhuri ya Kiislamu au kuifanya isalimu amri, na kwamba sasa inajiandaa kukabiliana na awamu mpya ya vita vya kiuchumi.

Akihutubia hafla ya kuadhimisha uzinduzi wa miradi 150,000 ya ajira, Aref amesema, Iran imeshinda kila mara majaribio yaliyofanywa na "mfumo wa kibeberu," unaoongozwa na Marekani, ya kutaka kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu.

Amebainisha kuwa, mkakati wa Iran katika miongo ya hivi karibuni umekuwa ni wa kujikita katika utumiaji wa teknolojia za hali ya juu ili kukidhi mahitaji ya nchi na ya watu wa eneo hili.

"Leo dunia imegundua kuwa iitwayo 'fimbo ya nyuklia' haikuwa chochote isipokuwa uwongo uliotolewa na utawala wa Kizayuni," ameeleza Aref na kuongeza kwamba, hoja hiyo imepoteza itibari wake.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amefafanua kuwa, baada ya kushindwa njama zake za awali, adui aligeukia makabiliano ya ana kwa ana ya kijeshi na Iran, akiamini kwamba watu wa Iran wangeingia mitaani kumuunga mkono.

"Lakini wananchi walithibitisha tena kwamba mahesabu ya Magharibi hayakuwa sahihi. Walisimama dhidi ya adui, na hatimaye adui akalazimika kuomba kusitisha mapigano."

Aref amekumbusha kuwa, lengo la kuipindua Jamhuri ya Kiislamu halijabadilika na kwamba adui alitaka kuiga mfano wa mapinduzi ya 1953 aliyoongoza dhidi ya serikali ya Iran kupitia operesheni ya pamoja ya kisiasa na kijeshi.

Amesema, adui aliamini kwamba, kama ilivyokuwa katika mapinduzi ya 1953, angeweza kufikia malengo yake kwa kutegemea "idadi kadhaa ya majambazi wa ngazi ya chini," lakini mahesabu hayo pia yalithibitika kutokuwa sahihi na badala yake mtaji wa kijamii wa Iran ukahamasishwa kuunga mkono Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran ameendelea kueleza kwamba, kwa kuwa mkakati wake wa kijeshi umeshindwa, adui sasa amejikita kwenye medani za kiuchumi na kijamii.

Amesema, Iran sasa imeingia katika vita vya kiuchumi, ambapo wapinzani wake wanaamini vikwazo na mzingiro vinaweza kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu.

"Tunaamini kwamba tumeingia katika vita vya kiuchumi," ameeleza Aref na kuongezea kwa kusema: "dhana ya adui ni kwamba kwa vikwazo na mzingiro anaweza kulihitimisha faili la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuupigiaha magoti Mfumo. Lakini sisi tunazo njia mpya za kutosha za baharini, ardhini na njia za reli na hatuna wasiwasi".

Amesisitiza: "tuna hakika katika medani hii pia adui atashindwa", kwa sababu hana wenzo mwingine zaidi ya vikwazo vikali na vya kidhalimu alivyokwishavitumia hapo kabla dhidi ya Iran…/