Kuanzia Reuters hadi The New York Times: Ushahidi wa Kushambuliwa Sherehe ya Harusi huko Kuhestak kwa Silaha za Marekani
Kitendo cha kikatili cha Marekani huko Kuhestak, Sirik, kusini mwa Iran, hakiwezi tena kufichwa nyuma ya simulizi kinzani zinazoenezwa kuhusu vita. Vyombo vya habari vya Magharibi, wataalamu, na wanasiasa sasa wanazungumzia hadharani ushahidi unaoonyesha kuwa silaha za Marekani zilitumika kushambulia moja kwa moja sherehe ya harusi, na kusababisha vifo na majeraha kwa raia waliokuwa wakishiriki sherehe hiyo.
Katika uchambuzi wa silaha hizo, na kwa kutegemea picha na video zilizothibitishwa pamoja na maoni ya wataalamu wanne huru, shirika la Reuters limehitimisha namna mlipuko na uharibifu uliotokea eneo la tukio unavyoendana na shambulio la moja kwa moja la bomu la Marekani lenye uzito wa pauni 500. Mtaalamu mmoja wa vilipuzi amefafanua suala hilo kwa kusema: "Ushahidi unaashiria matumizi ya bomu la Marekani lenye uzito wa pauni 500 linalodondoshwa kutoka angani."
Maelezo haya yanathibitishwa zaidi na uchambuzi huru uliofanywa na gazeti la The New York Times. Kwa kulinganisha picha za satelaiti, video zilizothibitishwa, na mabaki ya silaha, gazeti hilo limebaini kuwa vipande vilivyopatikana eneo la tukio vinafanana na vile vya bomu linaloongozwa la JSOW la Marekani. Trevor Ball, mtaalamu wa zamani wa uteguzi wa mabomu na vilipuzi katika Jeshi la Marekani, alichunguza mabaki hayo na kubaini kuwa sehemu ya mkia na sehemu za mwili wa bomu hilo ni za aina hiyo hiyo ya silaha. Vyombo viwili vikuu vya habari vya Magharibi, chunguzi mbili huru, na rundo la ushahidi wa picha na silaha sasa vimefikia hitimisho moja: Silaha ya Marekani ilishambulia jengo la makazi ambapo watu walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya sherehe ya harusi.
Hata hivyo, umuhimu wa tukio la Kuhestak unavuka mipaka ya ripoti za vyombo vya habari. Mara hii, sauti za ukosoaji zimejitokeza pia kutoka ndani ya mfumo wa kisiasa na kijeshi wa Marekani. Wes J. Bryant, afisa wa zamani wa Pentagon aliyeshughulikia tathmini ya madhara kwa raia na mchambuzi wa jinai za kivita, ametoa majibu yafuatayo alipoulizwa, iwapo Marekani iliwalenga raia kwa makusudi nchini Iran: "Ndio." Akiegemea uzoefu wake ndani ya mfumo wa kijeshi wa Marekani, amesema kuwa Washington "huhatarisha na kuua raia kiholela na bila kujali lolote" wakati wa operesheni zake za kijeshi. Huku si kukiri kwa kawaida kisiasa. Mzungumzaji si mtu wa nje ya mfumo wa kijeshi wa Marekani, bali ni mtu aliyewahi kuwa na jukumu muhimu la kutathmini madhara kwa raia katika Pentagon. Hivyo, ushahidi wake kuhusu taratibu za kufanya maamuzi na mifumo ya uwajibikaji katika operesheni za kijeshi za Marekani una uzito wa kipekee.
Katika uwanja wa siasa, mbunge wa Marekani Delia Ramirez ameeleza ukweli huo huo kwa mtazamo tofauti. Ameandika kufuatia shambulio la Kuhestak kwamba: "Kuanzia Palestina hadi Iran, mabomu yetu yanaua wanawake na watoto wasio na hatia." Amesisitiza zaidi kuwa Bunge haliwezi kuendelea kupuuza "uhalifu wa kivita wa Trump na Hegseth." Huenda msemo huu ukawa ndio muhtasari ulio wazi zaidi wa yaliyotokea Kuhestak: "Mabomu yetu." Si bomu lisilojulikana, wala silaha yenye asili isiyojulikana; bali ni bomu ambalo mbunge wa Marekani analihusisha na nchi yake mwenyewe, huku akizungumzia wakati huo huo wanawake na watoto waliouawa kwa mabomu hayo.
Kuunganishwa kauli hizi kunatoa picha iliyo wazi zaidi. Shirika la Reuters linazungumzia zana za kivita za Marekani. Gazeti la The New York Times linabainisha mabaki ya silaha za Marekani. Mtaalamu wa zamani wa Jeshi la Marekani anahusisha ushahidi huo na bomu la Marekani. Afisa wa zamani wa Pentagon anazungumzia jinsi Marekani inavyowaweka raia hatarini na kuwaua kinyama. Mbunge wa Marekani pia amefichua mauaji ya wanawake na watoto yaliyosababishwa na "mabomu yetu." Hii si simulizi ya Iran pekee kuhusu shambulio la Marekani; ni tukio lililothibitishwa na nchi za Magharibi zenyewe, kupitia ushahidi na kauli zao zenyewe.
Kuhestak si jina tu la mji ulioko kusini mwa Iran; ni ushahidi unaoanika wazi pengo lililopo kati ya kauli za nchi za Magharibi kuhusu haki za binadamu na uhalisia wa vita vinavyoendeshwa na Marekani. Katika tukio hili, wahanga hawakuwa kwenye uwanja wa vita, bali walikuwa nyumbani katikati ya sherehe ya harusi. Wanawake na watoto waliuawa na kujeruhiwa, huku mabaki ya silaha za Marekani yakionekana katikati ya vifusi. Hivyo, dunia sasa inakabiliana na mtenda jinai ambaye hawezi tena kujificha nyuma ya pazia la kufunika ukweli. Jinai ya Marekani huko Kohestak si tukio nadra, inafichua sura halisi ya vita vya Marekani, vita ambavyo vinalenga kutimiza malengo yake ya kutaka kutawala dunia kupitia mauaji, jinai, ugaidi na uharibifu.