Makombora ya Balistiki ya IRGC yalazimisha meli za Kivita za Marekani kutoroka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141242-makombora_ya_balistiki_ya_irgc_yalazimisha_meli_za_kivita_za_marekani_kutoroka
Kikosi cha Anga za Juu cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimerusha makombora kadhaa ya balistiki kuelekea kwenye manowari mbili za Marekani ikiwemo ile yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita na kuzilazimu kutoroka. Meli hizo za kivita zilikuwa zikishiriki katika mzingiro haramu wa baharini wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2026-09-06T04:23:34+00:00 )
Sep 06, 2026 04:20 UTC
  • Kombora la Balistiki la Iran
    Kombora la Balistiki la Iran

Kikosi cha Anga za Juu cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimerusha makombora kadhaa ya balistiki kuelekea kwenye manowari mbili za Marekani ikiwemo ile yenye uwezo wa kubeba ndege za kivita na kuzilazimu kutoroka. Meli hizo za kivita zilikuwa zikishiriki katika mzingiro haramu wa baharini wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumamosi, IRGC ilieleza kuwa kikosi hicho kilitekeleza shambulio hilo la kulipiza kisasi dhidi ya meli hizo za kivita “zinazoomilikiwa na jeshi vamizi na lenye kuua watoto la Marekani, ambalo limekuwa likizisumbua meli za kibiashara za Iran na kushiriki katika mzingiro huo dhalimu.”

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Baada ya kupata uharibifu mkubwa na kwa hofu ya kupokea pigo jingine la kulipiza kisasi, meli hizo mbili za kivita zililazimika kukimbia kutoka eneo la makabiliano.”

Wakati huo huo, Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Marekani (CENTCOM) ilikiri kwamba meli zake za kivita zilikumbana na “mashambulizi mfululizo” kutoka upande wa Iran.

Akiakisi ungamo hilo, msemaji wa IRGC alibainisha jinsi “adui huyo mchokozi, ambaye kwa miaka mingi alitamba katika ukanda huu kwa majivuno ya uongo na madai matupu, leo amelazimika kukiri rasmi kwamba meli mbili za kivita za Jeshi la Majini la Marekani zimeshambuliwa.”

IRGC imesema: “Ungamo la CENTCOM linalothibitisha operesheni hii ni ushahidi hai wa kushindwa kimkakati kwa adui na thibitisho tosha la uwezo mkubwa wa kishambulizi wa IRGC.”

Kadhalika, IRGC imesisitiza kuwa jeshi hilo pamoja na vikosi vingine vya Ulinzi na Usalama vya Iran vimeshikamana imara katika kutetea mamlaka kamili ya nchi na usalama wa Jamhuri ya Kiislamu.

Hapo awali, IRGC ilikuwa imeweka hadharani kanda za video ambazo hazikuwahi kuonekana hapo kabla, zikionesha hatua madhubuti zilizochukuliwa dhidi ya meli zilizokiuka sheria katika Lango Bahari la Hormuz; hatua iliyofichua uongo wa madai ya Marekani kuhusu kutoa ulinzi madhubuti kwa meli zinazopita kinyume cha sheria kwenye njia hiyo muhimu ya majini.

IRGC iimeonya kwamba: “Marekani ndiyo tishio kubwa zaidi kwa usalama wa mataifa ya ukanda huu na biashara ya baharini; operesheni za Marekani za kutoa ulinzi na kusindikiza meli si chochote bali ni ghilba na uongo mtupu!”

Kabla ya kutolewa kwa kanda hizo za video, jeshi hilo pia lilikuwa limetangaza kushambulia meli tatu zilizokuwa na mafungamano na Marekani pamoja na meli tatu za mafuta zilizokiuka mipaka, ikiwa ni jibu la kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya awali ya Marekani dhidi ya meli za mafuta za Iran.