Meja Jenerali Rezaei: Iran itaainisha 'eneo jipya la marufuku' nje ya Mlango-Bahari wa Hormuz
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) amesema, eneo jipya la marufuku nje ya Mlango-Bahari wa Hormuz litatangazwa katika siku zijazo, akionya kwamba chombo chochote kitakachoingia katika eneo hilo bila mashauriano na Tehran kitawekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Iran.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni Jumapili usiku, Meja Jenerali Mohsen Rezaei, amebainisha kuwa eneo hilo "litaanzia kwenye mstari wa mzingiro uliowekwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani hadi sehemu kadhaa za Ghuba ya Uajemi," kuelekea kwenye bandari za upakiaji mizigo.
Rezaei amesisitiza kuwa, meli zinazoelekea kwenye mlango-bahari kutoka pande zote mbili na kuingia katika eneo hilo la marufuku lililotengwa, zitakabiliwa na matatizo ya bima na ya ruhusa ya upitaji katika siku zijazo.
Aidha, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametamka kinagaubaga kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz "umefungwa kikamilifu na uko chini ya udhibiti wa vikosi vya ulinzi," na kuyaelezea madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba njia hiyo ya kimkakati ya majini ingali iko wazi kuwa ni "uongo mkubwa".
Rezaei amefafanua kuwa, kabla ya Iran kuufunga mlango-bahari huo, zaidi ya meli 100 zilizobeba zaidi ya tani milioni 100 za mizigo zilikuwa zikipita hapo kila siku, lakini sasa, ni meli saba hadi nane tu zinazobeba bidhaa muhimu kwa ajili ya Iran ndizo zinazopita katika njia hiyo ya majini.
"Wamarekani wanajaribu kupenyeza meli tano hadi sita kimagendo kwa gharama kubwa, lakini kikawaida meli hizi hushambuliwa," ameeleza Rezaei na kuongeza kwamba Iran haijaamua kuzizamisha meli hizo zinazovukishwa kimagendo, kwa sababu hubeba mafuta na zitachafua mazingira ya eneo hilo.
Katika mahojiano hayo ya televisheni, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ametangaza kwamba hati ya makubaliano na Oman kuhusu ushoroba mpya wa upitaji meli utakaotumika katika Mlango-Bahari wa Hormuz itasainiwa katika siku zijazo, ambapo uingiaji na utokaji kupitia ujia huo utakuwa chini ya usimamizi kamili wa Iran.
Aidha amesisitiza kuwa, Tehran haitatoa ahadi yoyote ya kuifungua tena njia hiyo ya majini mpaka pale Washington itakapokomesha vitisho na uchokozi na kurejesha imani kwa Iran…/