Qalibaf aukejeli utabiri wa Waziri wa Hazina wa Marekani kuhusu bei ya mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141276-qalibaf_aukejeli_utabiri_wa_waziri_wa_hazina_wa_marekani_kuhusu_bei_ya_mafuta
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amepuuzilia mbali utabiri wa Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, kwamba bei ya mafuta itashuka hadi dola 40 kwa pipa, akiutaja kuwa “ni mawazo na ndoto.”
(last modified 2026-10-14T04:35:26+00:00 )
Sep 07, 2026 11:17 UTC
  • Qalibaf aukejeli utabiri wa Waziri wa Hazina wa Marekani kuhusu bei ya mafuta
    Qalibaf aukejeli utabiri wa Waziri wa Hazina wa Marekani kuhusu bei ya mafuta

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amepuuzilia mbali utabiri wa Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, kwamba bei ya mafuta itashuka hadi dola 40 kwa pipa, akiutaja kuwa “ni mawazo na ndoto.”

Qalibaf amesema hayo akijibu kwa kejeli udhaifu wa kiuchumi wa Marekani katika maeneo matano.

Majibu makali ya Qalibaf, yaliyowasilishwa kwa mtindo wa kejeli kama “mazoezi ya kujipasha moto” kwa Bessent, yanaibainisha hali tete ya uchumi wa Marekani licha ya kile kinachoelezwa kuwa ni vita vya kisaikolojia vinavyoendeshwa na Washington. Qalibaf ameangazia mfumuko wa bei, uuzaji wa hati fungani za madeni ya Marekani na uhaba wa wafanyakazi, mambo ambayo yanakinzana na simulizi za utawala wa Marekani kuhusu uchumi wake kuwa uko tayari “kupaa”.

Spika wa Buunge la Iran alishiriki picha ya kejeli inayoonyesha Bessent akiwa “anapaa” na kisha “akianguka bila kudhibitiwa,” ikiwa na maelezo yanayosema: “Jitayarishe kuruka; unahitaji kujipasha moto vizuri kabla ya kupaa!”

Kisha alitaja mambo matano: bei ya dizeli nchini Marekani kufikia viwango vya juu kabisa, Japan kuuza hati fungani za Serikali ya Marekani, Norway kuuza hati fungani zenye thamani ya dola bilioni 80, jeshi la Marekani kukabiliwa na uhaba wa waajiriwa wapya, na maafisa wa Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve) kuonya kuhusu mfumuko wa bei na viwango vya riba.

Mabadilishano ya kauli kati ya Qalibaf na Bessent ni zaidi ya majibizano ya kawaida kwenye mitandao ya kijamii; yanaakisi hali pana ya vita vya kiuchumi kati ya Iran na Marekani.

Wakati Washington ikijaribu kuonyesha nguvu kupitia operesheni za kisaikolojia, Tehran inaelekeza kwenye udhaifu unaoonekana wazi, ukiwemo kupanda kwa bei ya mafuta, nchi za kigeni kupunguza uwekezaji wao katika madeni ya Marekani, mizozo katika uajiri wa wanajeshi, pamoja na migongano ya kisera ndani ya Marekani.

Kwa kuchambua kwa ucheshi na usahihi hali iliyopo katiika uchumi wa Marekani, Qalibaf anaonyesha kwamba viongozi wa Iran hawatishwi na vitisho vya maneno, na kwamba simulizi ya Washington kuhusu uchumi wake “kuanza kupaa” inategemea zaidi mawazo ya kufikirika kuliko uhalisia.