Qalibaf aonya kuwa Iran italipiza kisasi kwa kushambulia rasilimali za nishati za Marekani
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ametoa onyo kali kwa Marekani kwamba shambulizi lolote dhidi ya rasilimali za mafuta na gesi za Iran litajibiwa kwa hatua sawa, akisisitiza kuwa makampuni na miundombinu ya nishati ya Marekani katika eneo hili iko katika hali sawa ya hatari.
Katika ujumbe aliousambaza kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumatatu, Qalibaf amebainisha udhaifu uliopo katika mnyororo wa uzalishaji wa nishati na kuonya kuwa shambulizi lolote la Marekani dhidi ya mali za Iran litajibiwa kwa mashambulizi dhidi ya maslahi ya Marekani.
Qalibaf ameandika: “Ni jambo rahisi: mnyororo wa uzalishaji wa mafuta na gesi hapa umeenea, unafikika, na uko wazi kushambuliwa.” Ameonya zaidi, “Makampuni ya mafuta na gesi ya Marekani katika maji haya na miundombinu yao inashiriki hatari hiyo hiyo. Shambulieni rasilimali zetu na nanyi mtashambuliwa.”
Ujumbe huo ulikuja kama jibu kwa vitisho vilivyotolewa na Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth, ambaye alikuwa ameonya kuwa Washington ingeharibu na kuzizamisha meli za mafuta za Iran iwapo Iran ingeshambulia meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani. Hegseth alidai kuwa meli za Iran hazina ulinzi na kudai kuwa ndege, meli, na nyambizi za Marekani zinaweza kuzishambulia meli hizo katika maeneo yaliyo chini ya mamlaka ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) na Kamandi ya Indo-Pacific.