Mafuta kwa Dola 40: Mgongano kati ya Ndoto ya Washington na Uhalisia wa Soko la Dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141292-mafuta_kwa_dola_40_mgongano_kati_ya_ndoto_ya_washington_na_uhalisia_wa_soko_la_dunia
Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran, amemjibu kwa kejeli, katika mtandao wa X, Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani anayeota kuwa bei ya mafuta itapungua hivi karibuni na kufikia dola 40.
(last modified 2026-09-08T09:26:02+00:00 )
Sep 08, 2026 09:20 UTC
  • Mafuta kwa Dola 40: Mgongano kati ya Ndoto ya Washington na Uhalisia wa Soko la Dunia

Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran, amemjibu kwa kejeli, katika mtandao wa X, Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani anayeota kuwa bei ya mafuta itapungua hivi karibuni na kufikia dola 40.

Kauli ya Scott Bessent, Waziri wa Fedha wa Marekani, kuhusu uwezekano wa bei ya mafuta kushuka hadi kufikia dola 40 kwa pipa, haiwezi kuchukuliwa kama utabiri wa kiuchumi wa kawaida tu katika soko la nishati. Maoni haya yana uzito mkubwa zaidi yakizingatiwa katika muktadha wa sera za kiuchumi na kijiopolitiki za serikali ya Marekani, ambapo mafuta ya bei nafuu yanaweza kusaidia pakubwa katika kupunguza mfumuko wa bei na gharama za nishati nchini humo, huku yakiongeza mashinikizo ya kiuchumi kwa nchi zinazouza mafuta, zikiwemo zile ambazo ni wapinzani wa Washington. Kwa mtazamo huu, jibu la Mohammad Bagher Ghalibaf, na namna alivyoitaja kauli ya Bessent kuwa ni "matarajio yasiyo na uhalisia", linaweza kuonekana kama pengo lililopo kati ya matarajio ya Marekani na uhalisia wa mambo katika soko la kimataifa la mafuta.

Uhalisia ni kwamba, tofauti na bidhaa nyingine nyingi, bei ya mafuta huathiriwa na mambo mengi mbalimbali na wala haiwezi kuainishwa kwa uamuzi wa serikali moja. Usambazaji na mahitaji ya dunia, viwango vya akiba, uwezo wa ziada wa uzalishaji, hali ya uchumi wa dunia, sera za OPEC na OPEC+, mabadiliko ya kijiopolitiki, gharama za uzalishaji, na matarajio ya soko, yote haya yana mchango katika kuamua bei ya mwisho ya mafuta. Kwa hivyo, hata kama Washington itafanikiwa kuathiri mwelekeo wa bei kupitia mashinikizo ya kisiasa, kidiplomasia au kiuchumi, lakini kushukisha bei ya mafuta hadi dola 40, na muhimu zaidi, kuifanya itulie katika kiwango hicho, kunahitajia mazingira na juhudi kubwa zisizo za kawaida.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imeibuka kama mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani, huku sehemu kubwa ya uzalishaji wake ikitokana na mafuta ya *shale*. Sekta hii huathiriwa sana na bei ya mafuta, ambapo kushuka kwa kasi na kwa muda mrefu kwa bei kunaweza kupunguza pakubwa faida ya makampuni, uwekezaji, na shughuli za uchimbaji, na hatimaye kupunguza viwango vya uzalishaji wa ndani nchini Marekani. Hali hii inaakisi mgongano wa kimsingi kati ya "mafuta ya bei nafuu kwa watumiaji" na "bei za juu za kutosha kuendeleza uzalishaji wa ndani", changamoto ya kusawazisha mambo ambayo serikali ya Marekani inalazimika kuishughulikia haraka.

Bila shaka, bei ya chini ya nishati ina mvuto mkubwa kwa serikali ya Marekani, ikizingatiwa mitazamo ya kiuchumi na kisiasa. Kushuka kwa bei ya mafuta na bidhaa zinazotokana na mafuta kunaweza kupunguza gharama za usafirishaji na uzalishaji, kuongeza uwezo wa familia kununua bidhaa, na kupunguza baadhi ya mashinikizo ya mfumuko wa bei. Kwa muktadha huu, mafuta ya bei nafuu yanaweza kuisaidia serikali ya Trump kusimamia uchumi wa ndani na hata kuongeza juhudi za kuridhisha umma.

Jibu la Ghalibaf pia linagusia soko la Dhamana za Hazina ya Marekani na mwenendo wa wamiliki wakuu wa dhamana hizo. Hili ni jambo muhimu kwa sababu sera ya kiuchumi ya Marekani haifanyi kazi katika ombwe. Washington hutegemea wawekezaji wa kigeni na benki kuu za mataifa mengine kufadhili nakisi yake ya bajeti. Kupungua kwa mahitaji ya dhamana za Hazina au kupanda kwa mapato yanayotokana na dhamana hizo, kunaweza kuongeza gharama za ukopaji kwa serikali ya Marekani. Hivyo, serikali ya Marekani lazima idhibiti mfumuko wa bei, viwango vya riba, deni la umma, ukuaji wa uchumi, na soko la dhamana kwa wakati mmoja, mambo ambayo si lazima yaelekee upande mmoja.

Suala la mfumuko wa bei lina umuhimu maalum katika muktadha huu. Ingawa kushuka kwa bei ya mafuta kunaweza kusaidia kupunguza baadhi ya mashinikizo ya mfumuko wa bei, sera za fedha na biashara pia huathiri mwenendo wa mfumuko wa bei. Hivyo, mvutano unaweza kutokea kati ya malengo ya Wizara ya Fedha ya kutaka kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza gharama za nishati, na mambo yanayozingatiwa na Hifadhi ya Shirikisho kuhusu udhibiti wa mfumuko wa bei na viwango vya riba. Kwa ufupi, uchumi wa Marekani unakabiliwa na masuala kadhaa tata ya vigezo vinavyofungamana, ambapo kushuka kwa bei ya mafuta hakuwezi kufuatiliwa bila kuzingatia athari zake kwa sekta zingine za uchumi. Bei ya chini ya mafuta inaweza pia kutafsiriwa kama sehemu ya mashinikizo ya kiuchumi ambayo Marekani huyatoa dhidi ya wapinzani wake.  Kauli ya Bessent inaweza kuchukuliwa kama sehemu ya mkakati mpana zaidi wa kutumia uchumi na nishati kama chombo cha kuongeza mashinikizo dhidi ya wapinzani wa Marekani. Hata hivyo, ukubwa wa taathira za hatua hiyo kwa Iran utategemea mambo kama vile kiasi cha mauzo ya nje, hali ya soko, gharama za uzalishaji na usafirishaji, viwango vya kubadilisha fedha na uwezo wa Iran wa kusimamia mapato yake ya mafuta.

Wakati huo huo, ni lazima tutafautishe kati ya "uwezekano wa muda mfupi wa bei ya mafuta kuwa dola 40" na "uwezekano wa bei hiyo ya dola 40 kudumu." Katika hali kama hiyo, wazalishaji hawatabaki bila kuchukua hatua, bali wanaweza kukabiliana na hali hiyo kwa kupunguza uzalishaji pamoja na uwekezaji.

Hivyo, ujumbe mkuu wa jibu la Ghalibaf ni kwamba Washington lazima ipime gharama na changamoto zinazohusiana na bei ya mafuta kuwa dola 40 kabla ya kuichukulia hali hiyo kama jambo linalowezekana kivitendo. Ingawa mafuta ya bei nafuu yanaweza kuwa jambo linalotamanika kwa watumiaji wa Marekani, lakini yanaweza pia kuathiri sekta ya mafuta ya 'shale', uwekezaji katika nishati, soko la dhamana za serikali, na hata uthabiti wa uchumi wa dunia. Hivyo basi, bei ya mafuta ya dola 40 si lengo rahisi linaloweza kufikiwa kupitia hatua za kisera; bali ni hali tata ambayo kufikiwa na kudumu kwake kunategemea mchanganyiko wa mazingira ya kiuchumi, kifedha na kijiopolitiki.