"Kutengwa Kiuchumi": Je, ni Onyesho la Nguvu au Dhihirisho la Mapungufu ya Marekani?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141318-kutengwa_kiuchumi_je_ni_onyesho_la_nguvu_au_dhihirisho_la_mapungufu_ya_marekani
Huku watawala wa Marekani wakiitishia Iran kuwa wataiwekea vikwazo vya kiuchumi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma, CNN imeripoti kuwa utekelezaji wa tahadhari na wa hatua kwa hatua wa kampeni ya "kutengwa kiuchumi" hautakuwa na athari yoyote kwa Iran, taifa ambalo limestahimili aina mbalimbali za vikwazo kwa miaka hamsini.
(last modified 2026-09-09T08:26:44+00:00 )
Sep 09, 2026 08:22 UTC

Huku watawala wa Marekani wakiitishia Iran kuwa wataiwekea vikwazo vya kiuchumi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma, CNN imeripoti kuwa utekelezaji wa tahadhari na wa hatua kwa hatua wa kampeni ya "kutengwa kiuchumi" hautakuwa na athari yoyote kwa Iran, taifa ambalo limestahimili aina mbalimbali za vikwazo kwa miaka hamsini.

Hivi karibuni Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, aliwaagiza wanadiplomasia wa Marekani kote duniani kuwaambia wenyeji wao kuwa lazima wakate uhusiano na Iran na kufunga mara moja matawi yanayofanya kazi ya benki za Iran. Tarehe 4 Septemba, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuwa imelenga benki moja ya Uturuki na kampuni tanzu zake. Badala ya kuanzisha vikwazo vya mara moja, Washington imeamua kutekeleza vita vyake vya kiuchumi dhidi ya Iran hatua kwa hatua.

Wimbi jipya la vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran, vilivyopewa jina la "Operesheni ya Kutenga Kiuchumi", linakusudiwa kuibana zaidi Iran kiuchumi na kudhoofisha uwezo wake uliosalia wa kufanya biashara na mataifa ya nje, kwa kuyalazimisha yakate uhusiano wa kiuchumi na kibenki na Tehran.

Hata hivyo, namna sera hii inavyotekelezwa, hasa utekelezaji wa vikwazo kwa tahadhari, hatua kwa hatua, na kwa vipande-vipande, unaonyesha tofauti kubwa iliyopo kati ya kauli za Washington kuhusu "mashinikizo ya kiwango cha juu" na uwezo wake halisi wa kuendesha vita kamili vya kiuchumi dhidi ya Tehran. Muhimu zaidi, tahadhari ya Marekani haitokani tu na masuala ya kisheria au hofu ya madhara ya kisiasa, bali inatokana na vizingiti halisi vya nguvu ya kiuchumi ya Marekani na gharama kubwa zinazohusiana na kuweka vikwazo vya ziada dhidi ya washirika muhimu wa kibiashara wa Iran.

Ukweli ni kwamba vikwazo vya Marekani vinaweza kufanikiwa tu pale Washington itakapoweza kulazimisha mtandao mpana wa nchi, benki, makampuni, na waamuzi wa kibiashara kutekeleza kikamilifu masharti yake, suala ambalo halionekani popote kwa sasa.

China ni mshirika muhimu wa kibiashara wa Iran na pia ni nguvu kubwa ya kiuchumi duniani. Hivyo, kuweka vikwazo vikali dhidi ya makampuni na taasisi za China zinazoshirikiana na Iran kunaweza kutumbukiza uhusiano wa kiuchumi na kisiasa wa Washington na Beijing katika mgogoro mkubwa. Marekani haiwezi, kuilazimisha China kukata kabisa uhusiano wake na Iran, bila kupima gharama za hatua kama hiyo na kwa kutegemea vikwazo pekee. Kwa hakika, kuyawekea vikwazo mashirika ya China kunaweza, kuchochea mzozo wa kiuchumi kati ya Marekani na China badala ya kuitenga Iran, na hivyo kudhoofisha zaidi ushawishi wa Washington ndani ya mfumo wa uchumi wa kimataifa.

Mazingatio hayo hayo yanahusu pia nchi kama vile Pakistan na Oman. Mbali na uhusiano wao wa kiuchumi na Iran, nchi hizi zina majukumu muhimu katika mienendo ya kisiasa na kidiplomasia ya kikanda; hasa wakati wa vita na migogoro, ambapo zinaweza kutumika kama njia za mawasiliano na upatanishi kati ya Tehran na Washington. Hivyo, Marekani inakabiliwa na mkanganyiko wa kimsingi. Kwa upande mmoja, inataka kutishia kuweka vikwazo dhidi ya upande wowote unaofanya biashara na Iran ili kuongeza mashinikizo ya kiuchumi, huku kwa upande mwingine, ikihitaji ushirikiano wa baadhi ya nchi hizo hizo ili kumaliza migogoro na kudumisha njia za kidiplomasia. Kuziadhibu nchi hizi kunaweza kudhoofisha nguvu ya kidiplomasia ya Marekani, na huenda kukafanya gharama za kisiasa kuwa kubwa kuliko faida za kiuchumi. Sababu nyingine muhimu ni hatari inayotokana na matumizi ya kupindukia ya vikwazo vya daraja la pili (secondary sanctions). Kimsingi, vikwazo hivi hutumika kama njia ya kuwalazimisha wengine wachague kati ya kushirikiana na Iran au kupata fursa ya kutumia mfumo wa kifedha wa Marekani. Hata hivyo, matumizi ya mara kwa mara na makubwa ya zana hii yanaweza kudhoofisha itibari na nguvu yake. Ikiwa nchi zitaona kuwa Washington inazidi kutumia vibaya nguvu yake ya kifedha kuwaadhibu washirika wao wa kibiashara, zitapata motisha zaidi ya kuanzisha mifumo huru ya kifedha, kutumia sarafu zisizo za dola, na kubuni njia za biashara zilizo nje ya udhibiti wa Marekani. Hivyo, Marekani inakabiliwa na hali kinzani katika kutekeleza vikwazo vikubwa dhidi ya washirika wa Iran. Kadiri inavyotumia nguvu yake ya kuweka vikwazo, ndivyo unavyoongezeka uwezekano wa nchi hizo kujitahidi kupunguza utegemezi wao kwa Marekani. Kwa upande mwingine, uzoefu wa miongo kadhaa ya vikwazo dhidi ya Iran umevuruga kabisa mahesabu ya Washington. Kwa miaka mingi, na kutokana na mashinikizo ya vikwazo, uchumi wa Iran umeunda mbinu za kudumisha biashara, kukwepa vikwazo vya kifedha, kutumia watu wa kati, na kutumia njia mbalimbali za usafirishaji wa bidhaa nje na ndani ya nchi. Hivyo, vikwazo vipya vinaweza kuwa na matokeo ya maana iwapo tu vitalenga kwa wakati mmoja mitandao hiyo yenye matabaka kadhaa, jambo linalohitajia gharama kubwa za kiintelijensia, kisiasa na kiuchumi, na ambalo ni vigumu sana kulitekelezeka kivitendo. Kwa mtazamo huu, hatua zinazochukuliwa hatua kwa hatua katika "operesheni za kutenga kiuchumi" hazipaswi kuchukuliwa kama mbinu za kawaida tu kiutendaji, bali kama kielelezo cha vikwazo vya kimkakati vinavyoikabili Marekani. Washington inataka kuonyesha kuwa bado ina uwezo mkubwa wa kutoa mashinikizo makubwa ya kiuchumi kimataifa, lakini wakati huo huo inataka kuepuka kunasa kwenye migogoro ya kiuchumi na kisiasa inayoweza kuidhuru. Hivyo kuiwekea vikwazo benki ndogo ya Uturuki au makampuni mahususi, badala ya kuweka vikwazo jumla dhidi ya washirika wakuu wa Iran, ni hatua yenye gharama nafuu zaidi, inayotoa ujumbe wa kisiasa wa kuweka mashinikizo bila ulazima wa kusababisha mgongano mkubwa na mataifa makubwa au washirika wa kikanda wa Iran. Kiuhalisia, umuhimu wa "operesheni za kutenga kiuchumi" ni jaribio la kupima uwezo halisi wa Marekani wa kutumia nguvu zake za kifedha katika kutoa mashinikizo ya kijiopolitiki. Hivyo, tahadhari inayochukuliwa na Marekani katika kuwaadhibu wale wanaokiuka vikwazo dhidi ya Iran inaonyesha wazi kuwa vikwazo vina gharama na mipaka yake. Hivi sasa, Marekani inakabiliwa na changamoto ya kupima kati ya kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran na kudumisha uhusiano na washirika pamoja na mataifa muhimu kiuchumi na kidiplomasia, uwiano unaoonyesha kuwa, ingawa hatua ya "kuitenga Iran kiuchumi" inaweza kuwa na madhara kwa Iran, lakini madhara hayo si lazima yawe na uwezo wa kuitenga Tehran kutoka kwenye mfumo wa uchumi wa kikanda na kimataifa.