Shambulio la Marekani dhidi ya Meli za Mafuta za Iran: Mvutano Wahama kutoka Shinikizo la Kiuchumi hadi Mapigano ya Kijeshi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza kupitia taarifa kuwa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayatasita kutumia haki yake ya kimsingi ya kujilinda kisheria na kwamba yatajibu vikali na ipaswavyo kitendo chochote cha uchokozi wa kijeshi wa adui.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na shambulio la jeshi la Marekani dhidi ya meli zake za mafuta inaangazia kanuni muhimu ya sera ya ulinzi ya Iran: Uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya maslahi ya Iran hautapita bila kujibiwa. Shambulio dhidi ya meli za kibiashara za Iran katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman si tukio dogo la baharini tu. Shambulio hilo ni sehemu ya mashinikizo yanayoendelea ya Washington ambayo yamekuwa yakitekelezwa kwa miaka mingi kupitia vikwazo, mzingiro wa kiuchumi, na hatua zinazolenga mauzo ya mafuta ya Iran. Hata hivyo, tofauti muhimu ni kwamba mara hii, mashinikizo ya kiuchumi yameambatana na hatua za moja kwa moja za kijeshi dhidi ya sekta za biashara na nishati za Iran. Kwa vile meli za mafuta za Iran ni sehemu ya mnyororo wa kiuchumi wa nchi hii, Tehran inachukulia shambulio lolote dhidi ya meli zake kuwa ukiukaji wa maslahi ya taifa na mamlaka ya Iran.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza jambo hili, ikielezea hatua hiyo ya Marekani kama mwendelezo wa "uchokozi wa kijeshi, mzingiro wa majini, na vita vya kiuchumi" dhidi ya Iran. Umuhimu wa suala hili unatokana na ukweli kwamba hakupaswi kuwepo na tofauti kati ya vita vya kiuchumi na hatua za kijeshi zinazolenga biashara na nishati. Marekani inapotumia nguvu za kijeshi kuzuia mtiririko wa bidhaa zinazouzwa nje na biashara ya Iran, majibu yake yanaweza kuvuka mipaka ya kidiplomasia na kiuchumi na kuhamia kwenye uwanja wa vita vya kijeshi.
Hoja nyingine muhimu katika taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ni tangazo kwamba vituo na miundombinu ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan, pamoja na meli za kivita za Marekani zinazokaribia eneo hili vitashambuliwa. Sehemu hii ya taarifa inatoa ujumbe wa kimkakati kwa Washington na washirika wake wa kikanda kwamba Iran itawajibisha mhusika wa moja kwa moja na msaidizi wake mkuu kwa hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya maslahi yake kutokea ardhi, vituo, au miundombinu ya mataifa ya eneo. Msimamo huu unatoa changamoto kubwa kwa mfumo wa usalama wa Marekani katika eneo. Katika miongo michache iliyopita, Washington imeanzisha mtandao mpana wa kambi za kijeshi, vikosi, na zana za kivita katika eneo la Asia Magharibi ili kutumika kama njia ya kuwatishia mahasimu wake na hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na eti kulinda usalama wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo, kama tulivyoshuhudia katika vita vya karibuni vya utawala ghasibu wa Israel na Marekani dhidi ya Iran, mtandao huo huo haukusaidia lolote katika kudhamini usalama unaodaiwa, bali wenyewe uligeuka kuwa shabaha ya mashambulio makali ya Iran na hivyo kuisababishia Marekani maafa na hasara kubwa za kijeshi. Kadiri idadi ya kambi na vituo vya kijeshi inavyoongezeka, ndivyo eneo la kijiografia ambapo Marekani inaweza kudhurika linavyozidi kupanuka.
Onyo lililotolewa na Meja Jenerali Ali Abdollahi, Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Iran, kwamba uchokozi wowote dhidi ya meli za mafuta za Iran utajibiwa kwa mashambulizi makali dhidi ya kambi za Marekani katika eneo, linafafanua wazi mantiki hii. Ujumbe wa Tehran ni kwamba usalama wa vikosi na kambi za Marekani hauwezi kutenganishwa na hatua za kijeshi ambazo nchi hiyo inazichukua dhidi ya Iran. Iwapo Washington italenga usalama wa biashara wa Iran, Iran nayo itachukulia usalama wa miundombinu ya kijeshi ya Marekani katika eneo kama sehemu ya mlingano wa hatua zake za kulipiza kisasi.
Wakati huo huo, hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ya kuhusisha suala hilo na Umoja wa Mataifa pamoja na majukumu ya Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wake inaashiria kuwa Iran inajaribu kuelekeza mashambulizi hayo katika muktadha wa sheria za kimataifa. Kanuni ya kujilinda kihalali dhidi ya uchokozi wa kijeshi ni nguzo muhimu ya Hati ya Umoja wa Mataifa, na kwa kuashiria kanuni hiyo, Tehran inachukulia hatua yake ya kijeshi kama hatua halali ya kujibu uchokozi unaofanywa na maadui. Hatimaye, suala la meli za mafuta linavuka mipaka ya mzozo wa kawaida wa baharini. Kwa kushambulia meli za Iran, Marekani inalenga kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran kufikia kiwango kipya; hata hivyo, hatua hii inaweza pia kuigeukia Marekani yenyewe kwa sura ya gharama za kijeshi. Ujumbe unaotolewa na taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran uko wazi: Marekani haiwezi kushambulia maslahi ya Iran na kutarajia kuwa majibu ya Iran yatadhibitiwa tu ndani ya uwanja ulioainishwa na Washington yenyewe.