Wairani 352,983 washtaki Marekani na Israel kwa vita vya kwanza dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141426-wairani_352_983_washtaki_marekani_na_israel_kwa_vita_vya_kwanza_dhidi_ya_iran
Kesi ya kwanza ya madai iliyofunguliwa na familia za waathiriwa wa “Vita vya Siku 12” vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran mwezi Juni 2025, ilisikilizwa Jumapili asubuhi katika Mahakama ya Iran jijini Tehran.
(last modified 2026-09-13T11:22:23+00:00 )
Sep 13, 2026 11:18 UTC
  • Iran yaanza kusikiliza kesi ya kihistoria dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni kufuatia “Vita vya Siku 12”
    Iran yaanza kusikiliza kesi ya kihistoria dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni kufuatia “Vita vya Siku 12”

Kesi ya kwanza ya madai iliyofunguliwa na familia za waathiriwa wa “Vita vya Siku 12” vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran mwezi Juni 2025, ilisikilizwa Jumapili asubuhi katika Mahakama ya Iran jijini Tehran.

Kesi hiyo iliongozwa na Jaji Majid Hosseinzadeh na kuhudhuriwa na Hassan Abdolianpour, Mkuu wa Kituo cha Wanasheria, Wataalamu Rasmi na Washauri wa Familia cha Idara ya Mahakama, pamoja na wadai na mawakili wao.

Kesi hiyo inahusisha raia 352,983 wa Iran ambao wamefungua zaidi ya mashtaka 110 kuhusiana na uharibifu wa mali na athari mbaya zilizosababishwa na mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran wakati wa vita hivyo vya siku 12, na hatua nyingine zilizofuata.

Wadai wanatafuta fidia kutoka kwa serikali ya Marekani, maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Kizayuni, na watu wengine pamoja na taasisi za kisheria zinazohusishwa na vitendo hivyo vya uchokozi. Mashtaka hayo pia yanalenga kuwawajibisha wahusika na kujenga kizuizi dhidi ya kurudiwa kwa vitendo kama hivyo.

Mwezi Juni 2025, utawala wa Kizayuni, ukishirikiana na Marekani, ulianzisha awamu ya kwanza ya uchokozi dhidi ya Iran, kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran huko Fordow, Natanz, na Isfahan. Vita hivyo, vilivyodumu kwa siku 12, vilikabiliwa majibu  madhubuti ya kulipiza kisasi ya majeshi ya Iran, jambo ambalo liliwalazimu maadui waombe usitishwaji vita.

Katika ufunguzi wa shauri hilo, Jaji Hosseinzadeh amesema kuwa wadai wameleta kesi zao kutokana na “uharibifu, madhara, na hasara za kimaadili zilizotokana na uchokozi dhidi ya mamlaka ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita hivyo vya siku 12 na vitendo vilivyofuata.”

Jaji ametaja sheria kadhaa za Iran kama msingi wa kisheria kwa mahakama za ndani kusikiliza kesi hizo.  Amesema kuwa chini ya sheria ya mwaka 2017 inayoshughulikia ukiukaji wa haki za binadamu na vitendo vya kigaidi vya Marekani katika eneo, taasisi za kijeshi na ujasusi za Marekani zinachukuliwa kuwa ni taasisi za kigaidi, na mashambulizi hayo yanaangukia chini ya vifungu husika.

Jaji Hosseinzadeh amesema suala kuu mbele ya mahakama ni ukiukaji wa ardhi na mamlaka ya Iran wakati wa Vita vya Siku 12, pamoja na vitendo haramu vilivyofuata vya utawala wa Kizayuni na Marekani, akiongeza kuwa maelezo na nyaraka za uthibitisho zimerekodiwa rasmi katika mwenendo wa kesi hiyo.