Waziri wa Ulinzi: Iran itakuwa na teknolojia ya kisasa zaidi katika vita vyovyote vipya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141436-waziri_wa_ulinzi_iran_itakuwa_na_teknolojia_ya_kisasa_zaidi_katika_vita_vyovyote_vipya
Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itakuwa na maendeleo makubwa zaidi ya kiteknolojia iwapo vita vingine vitazuka.
(last modified 2026-09-14T04:03:26+00:00 )
Sep 14, 2026 04:02 UTC
  • Brigedia Jenerali Majid Ibn al-Reza
    Brigedia Jenerali Majid Ibn al-Reza

Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itakuwa na maendeleo makubwa zaidi ya kiteknolojia iwapo vita vingine vitazuka.

Brigedia Jenerali Majid Ibn al-Reza ameyasema hayo siku ya Jumapili wakati akizungumza na wasimamizi wa mashirika ya viwanda chini ya Wizara ya Ulinzi, akijibu vitisho na maneno makali yanayoendelea kutolewa na baadhi ya maafisa wa serikali ya Marekani.

Aida amesema: “Baadhi ya maafisa wa Marekani wanadhani kuwa wanaweza kubadili msimamo wetu thabiti au kuitisha Jamhuri ya Kiislamu kwa kurudia vitisho vyao, lakini wanafanya kosa kubwa sana."

Ameongeza kuwa kuendelea kwa adui kutoa vitisho kama hivyo hakuakisi nguvu yoyote, bali ni ushahidi tosha wa kupooza kwa mifumo yao ya kijasusi na tathmini za kistratijia, na hatimaye, kuporomoka kwa fikra sahihi na hekima ndani ya uongozi wao.

Ibn al-Reza amesisitiza kuwa ni lazima adui afahamu ukweli huu “ulio wazi na ulio dhahiri kabisa” kwamba asithubutu kuongea na Iran kwa lugha ya vitisho na ubabe.

Amebainisha tena kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitilii maanani kabisa propaganda hizo, akizieleza kuwa ni “ujumbe au kauli za kisiasa tu” zisizo na nguvu yoyote halisi ya kijeshi ardhini.

Akiangazia mienendo ya kanda hiyo na matokeo ya siasa haribifu za Marekani na utawala wa Kizayuni, Kaimu Waziri huyo wa Ulinzi amesema: “Matukio na hali halisi tunayoishuhudia leo katika eneo hili ni zao la siasa zao potofu na mahesabu mabovu waliyoyafanya.”

Amefafanua kuwa Iran haijawahi kuwa tishio kwa nchi jirani wala kwa mataifa mengine ya kanda hii, na siku zote imekuwa makini kutofautisha kati ya marafiki wa kweli na mahasimu, huku ikidhihirisha mtazamo huo wa busara kwa vitendo katika nyakati na hali mbalimbali.

Jenerali Ibn al-Reza amethibitisha kuwa hivi sasa Iran ni “imara zaidi, yenye mshikamano mkubwa zaidi, na macho zaidi” kuliko wakati mwingine wowote katika historia yake. Ameongeza kuwa uwezo wa kiulinzi na kiteknolojia wa taifa la Iran  unazidi kusonga mbele kwa kutumia mafunzo na tajriba iliyopatikana uwanjani na katika medani za mapambano.

Kaimu Waziri huyo amehitimisha kwa kusema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inategemea utashi wake thabiti, vipaji vya wataalamu wa ndani ya nchi, na uwezo wake binafsi wa ndani ili kujihakikishia usalama na kutetea maslahi yake makuu.”