Jeshi la Iran laangusha ndege ya kivita isyo na rubani ya Marekani katika Lango la Hormuz
-
Droni ya MQ1
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa limetungua na kuiangamiza ndege nyingine isiyo na rubani (droni) ya kisasa ya kivita ya Marekani aina ya MQ-1 juu ya anga ya Lango-Bahari la Hormuz.
Ofisi ya Mahusiano ya Umma ya IRGC imesema katika taarifa yake rasmi siku ya Jumatatu kwamba ndege hiyo isiyo na rubani iligunduliwa na kutunguliwa na mfumo wa kisasa wa ulinzi wa anga unaoendeshwa na Kikosi cha Anga za Juu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kulingana na taarifa hiyo, operesheni hiyo ilitekelezwa kwa uratibu na chini ya uongozi wa mtandao jumuishi wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Taarifa hiyo ilibainisha: “Droni hiyo ya kisasa ya ujasusi ya MQ-1 ilifuatiliwa, ikazuiwa, na kuangamizwa kikamilifu angani juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz.”
Wiki iliyopita pia, kitengo cha ulinzi wa anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Artesh) kiliitungua droni nyingine ya kijeshi ya Marekani ya MQ-1 juu ya njia hiyo hiyo ya kistratejia ya Lango-Bahari la Hormuz.
Lango-Bahari la Hormuz limezidi kuwa uwanja mkuu katika vita na mashinikizo ya kichokozi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Uchokozi huo umeifanya Iran kuimarisha na kusisitiza udhibiti wake kamili wa kiusalama juu ya harakati zote za wanamaji ndani na pembezoni mwa lango-bahari hilo muhimu.
Katika muongo mmoja uliopita, vikosi vya kijeshi vya Iran vimefanikiwa kutungua au kuteka zana nyingi za kijeshi za thamani kubwa na za kisiri za Marekani, ikiwa ni pamoja na droni ya ujasusi ya kuteleza angani ya RQ-170 Sentinel, droni za kisasa za MQ-9 Reaper, pamoja na nyambizi ndogo ndogo zisizo na rubani na vyombo vya majini visivyo na rubani katika Ghuba ya Uajemi.
Teknolojia hizo zilizotekwa zimekuwa na mchango mkubwa na wenye taathira pana katika kuongeza kasi ya mafanikio ya viwanda vya ndani vya Iran katika uundaji wa ndege zisizo na rubani na mifumo ya kisasa ya baharini isiyo na rubani.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la habari la Bloomberg, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeangamiza zaidi ya droni 24 za aina ya MQ-9 tangu kuanza kwa uvamizi na vita vya kigaidi vya Marekani na utawala wa Kizayuni mwezi Februari mwaka huu. Idadi hiyo ni asilimia 20 ya hifadhi yote ya silaha hizo iliyokuwepo Pentagon kabla ya vita hivyo. Kwa gharama ya dola zaidi ya milioni 30 kwa kila ndege moja, jumla ya hasara iliyosababishwa kwa jeshi la Marekani inakadiriwa kufikia takriban dola bilioni 1.