Meli kubwa ya mafuta yalipuka baada ya kukanyaga mabomu ya majini kwenye njia haramu kusini mwa Hormuz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141470-meli_kubwa_ya_mafuta_yalipuka_baada_ya_kukanyaga_mabomu_ya_majini_kwenye_njia_haramu_kusini_mwa_hormuz
Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetangaza kuwa meli kubwa ya kubeba mafuta ghafi (supertanker) iliyojaribu kupita bila idhini katika eneo lililopigwa marufuku kusini mwa Lango Bahari la Hormuz imelipuka baada ya kukanyaga mabomu ya kutega majini, huku chombo hicho chote kikiwa kimeteketea na kufunikwa na miali mikubwa ya moto.
(last modified 2026-09-15T04:18:07+00:00 )
Sep 15, 2026 04:15 UTC
  • Meli ya mafuta ikiteketea
    Meli ya mafuta ikiteketea

Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetangaza kuwa meli kubwa ya kubeba mafuta ghafi (supertanker) iliyojaribu kupita bila idhini katika eneo lililopigwa marufuku kusini mwa Lango Bahari la Hormuz imelipuka baada ya kukanyaga mabomu ya kutega majini, huku chombo hicho chote kikiwa kimeteketea na kufunikwa na miali mikubwa ya moto.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa Jumatatu usiku, Kikosi cha Wanamaji cha IRGC kiliitambulisha meli hiyo kuwa ni Algaya, inayotambuliwa pia kama El Gaia, yenye nambari ya kimataifa ya usajili wa meli (IMO) 9325336.

Taarifa hiyo ya kijeshi imeeleza kuwa meli hiyo ya mafuta ilijaribu kupita katika njia isiyoidhinishwa na hatarishi mno licha ya maonyo ya wazi yaliyokuwa yametolewa hapo awali na mamlaka husika kuhusu hatari kubwa zilizopo katika mkondo huo.

Jitihada zote za kudhibiti na kuuzima moto huo mkubwa ziligonga mwamba, iliongeza taarifa hiyo, na kukiacha chombo hicho kikiwa kinateketea moto kikamilifu baharini.

Kikosi cha Wanamaji cha IRGC kimebainisha bayana kuwa tukio hilo lilikuwa tokeo lililotarajiwa la kupuuza sheria na kanuni za usalama wa bahari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika njia hiyo ya kimkakati ya baharini ambayo Iran iliiweka chini ya udhibiti kamili wa kiutendaji wa hali ya vita. Hatua hiyo ya Iran ilichukuliwa mara tu baada ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kuanzisha vita vya kichokozi na visivyo na msingi wowote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Taarifa ya IRGC imesema: “Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kinatangaza kwa msisitizo thabiti kuwa Lango Bahari la Hormuz limefungwa na linaendelea kubaki chini ya udhibiti wetu kwa kutegemea teknlojia za kisasa."

Iran imetoa indhari mara kwa mara kwa makampuni ya kimataifa ya meli kutofanya makosa ya kutegemea ahadi hewa na za hadaa za Marekani kuhusu eti uwepo wa “njia salama,” katika Lango la Hormuz. Iran imesisitiza kuwa meli yoyote inayoingia katika maeneo yaliyotegwa mabomu au yaliyopigwa marufuku, au inayong’oa nanga bila uratibu wa moja kwa moja na Mamlaka ya Lango-Bahari la Ghuba ya Uajemi, inajiingiza yenyewe, mabaharia wake na shehena zake katika maangamizi ya wazi.

Viongozi wa Iran wamepuuzilia mbali propaganda chafu za Marekani zinazolenga kurubuni meli za biashara kuelekea kwenye mikondo hatarishi ya maji, kwa lengo la kufunika aibu na kushindwa kwa jeshi la Marekani kufungua njia hiyo ya bahari ambayo haina udhibiti wala mamlaka nayo.

Kikosi cha Wanamaji cha IRGC kimehimiza kuwa kufuata taratibu na kanuni za Iran ni wajibu usioepukika, na kwamba majaaliwa ya chombo chochote kitakachokiuka amri na sheria za kiusalama za Lango-Bahari la Hormuz hayatakuwa tofauti na hatima ya meli zilizokwisha zuiliwa au kuteketezwa kwa moto.