Jeshi, IRGC: Iran inawakabili maadui ambao hakuna taifa jengine linalothubutu 'kuwafyatulia hata risasi moja'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141482-jeshi_irgc_iran_inawakabili_maadui_ambao_hakuna_taifa_jengine_linalothubutu_'kuwafyatulia_hata_risasi_moja'
Wasemaji wakuu wa Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wameashiria umoja usioweza kuvunjika kati ya matawi hayo mawili ya kijeshi na kutangaza kwamba Iran inavishambulia kwa mafanikio vikosi vya Marekani na Israel, vilivyojizatiti kwa silaha nzito, ambazo hakuna nchi nyingine yoyote duniani inayothubutu kukabiliana nazo.
(last modified 2026-09-15T11:41:21+00:00 )
Sep 15, 2026 11:38 UTC
  • Jeshi, IRGC: Iran inawakabili maadui ambao hakuna taifa jengine linalothubutu 'kuwafyatulia hata risasi moja'

Wasemaji wakuu wa Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wameashiria umoja usioweza kuvunjika kati ya matawi hayo mawili ya kijeshi na kutangaza kwamba Iran inavishambulia kwa mafanikio vikosi vya Marekani na Israel, vilivyojizatiti kwa silaha nzito, ambazo hakuna nchi nyingine yoyote duniani inayothubutu kukabiliana nazo.

"Tunasimama dhidi ya maadui wanaomiliki wingi mkubwa wa teknolojia na silaha. Hakuna nchi duniani inayothubutu kuwafyatulia hata risasi moja, lakini sisi tumesimama dhidi yao, tumewapiga, na hatukuwaruhusu kutimiza malengo yao," ameeleza Msemaji wa Jeshi Brigedia Jenerali Mohammad Akrami-Nia.

Matamshi hayo yametolewa wakati wa mkutano wa uratibu uliofanyika kwenye makao makuu ya Jeshi mjini Tehran, ambapo Akrami-Nia alitembelewa na Msemaji wa IRGC Brigedia Jenerali Hossein Mohebbi.

Mkutano huo ulijikita katika kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya habari na kuunganisha nguvu za utendaji kazi kati ya Jeshi na IRGC wakati huu vinapoendelea vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na Israel.

Katika mkutano huo, Brigedia Jenerali Mohebbi amelisifu Jeshi la Iran kuwa ni fahari ya taifa, na kulitaja kuwa ni taasisi yenye nguvu, ya wananchi na iliyo kali dhidi ya ubeberu.

Amelinganisha makabiliano ya sasa na Vita vya Iran na Iraq vya 1980-1988, ambavyo vinajulikana nchini Iran kama Vita vya Kwanza vya Kujihami Kutakatifu.

"Katika Vita vya Pili na vya Tatu vya Kujihami Kutakatifu, kama ilivyokuwa katika vita vya kwanza, Jeshi limekuwa chombo cha kujivunia," ameeleza Mohebbi akiashiria vita vya karibuni vya kukabiliana na Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel.

"Uelewa wa pamoja na ushirikiano wa pamoja kiutendaji kati ya Jeshi, IRGC, serikali, na wananchi wanaojitokeza mabarabarani lazima virekodiwe na kudumishwa milele katika historia," amehimiza Mohebbi na kusisitiza kwamba matumaini aliyokuwa nayo adui ya kupanda mbegu za mgawanyiko ndani ya Iran yameishia kwenye kukata tamaa kikamilifu.

Kwa upande wake, msemaji wa Jeshi Akrami-Nia ametilia mkazo maelezo hayo na kubainisha kwamba, muundo wa kamandi iliyoungana chini ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu umevuruga kampeni za vita vya kisaikolojia vya Washington.

"Adui alikuwa amewekeza matumaini yake katika kuleta migawanyiko ya ndani, lakini leo hii, umoja ulioanzishwa ndani ya nchi umemfikisha adui kwenye mkwamo," ameeleza msemaji wa jeshi na kuongeza kuwa mshikamano huo wa kitaifa ndio unaodhamini ushindi kamili wa mwisho…/