Iran yashika nafasi ya tatu duniani katika kutibu ugumba, yakamilisha mpango wa chanjo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141490-iran_yashika_nafasi_ya_tatu_duniani_katika_kutibu_ugumba_yakamilisha_mpango_wa_chanjo
Mkuu wa Shirika la Madaktari la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeshika nafasi ya kwanza duniani katika utoaji wa chanjo na nafasi ya tatu duniani katika kutibuu tatizo la ugumba.
(last modified 2026-09-16T02:58:06+00:00 )
Sep 16, 2026 02:56 UTC
  • Iran yashika nafasi ya tatu duniani katika kutibu ugumba, yakamilisha mpango wa chanjo

Mkuu wa Shirika la Madaktari la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeshika nafasi ya kwanza duniani katika utoaji wa chanjo na nafasi ya tatu duniani katika kutibuu tatizo la ugumba.

Kwa mujibu wa Pars Today, ikinukuu Shirika la Habari la Vijana wa Iran, Mohammad Raiszadeh, Mkuu wa Shirika la Madaktari la Iran, amesema kwa sasa zaidi ya madaktari 170,000 wanafanya kazi hapa nchini, huku uwiano wa madaktari kwa idadi ya watu ukiwa madaktari 19 kwa kila watu 10,000.

Kwa mujibu wa Raiszadeh, kwa kutegemea takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa uwiano wa madaktari kwa idadi ya watu duniani ni madaktari 16 kwa kila watu 10,000. Hivyo, amesema Iran iko katika hali nzuri zaidi ikilinganishwa na wastani huo.

Raiszadeh amesisitiza kuwa kwa sasa Iran inashika nafasi ya kwanza duniani katika kiwango cha chanjo kwa watu wake, huku ikiwa katika nafasi ya tatu duniani katika matibabu ya utasa. Aidha, amesema Iran inashika nafasi ya nne duniani katika upandikizaji wa ini na figo.

Ameongeza kuwa Iran pia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika upandikizaji wa vifaa vya kusaidia uwezo wa kusikia (cochlear implant) pamoja na kufanya upasuaji wa moyo na aina nyingine za upasuaji tata.

Mwezi Julai mwaka huu Taasisi ya Utafiti ya Royan ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitajwa kuwa miongoni mwa taasisi kumi zenye ushawishi mkubwa zaidi duniani katika masuala ya utafiti wa ugumba wa kiume na teknolojia ya usaidizi wa uzazi (ART) ikishika nafasi ya tisa kimataifa.

Hayo ni kwa mujibu wa uchambuzi wa kisayansi wa machapisho yaliyotolewa kati ya mwaka 2000 na 2019. Utafiti huo ulichambua matokeo ya kazi za kisayansi za miongo miwili kuhusu ugumba wa wanaume na teknolojia ya ART kote duniani, na kubainisha taasisi 10 zenye ushawishi mkubwa zaidi katika nyanja hiyo kulingana na utendaji wao wa kiutafiti na athari zake za kisayansi.