Zarif: Iran inapinga silaha za aina yoyote za kemikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i31250
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa moja ya misingi mikuu ya Iran ni kupinga kikamilifu kuzalisha na kutumia silaha za aina yoyote za kemikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 02, 2017 15:18 UTC
  • Zarif: Iran inapinga silaha za aina yoyote za kemikali

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa moja ya misingi mikuu ya Iran ni kupinga kikamilifu kuzalisha na kutumia silaha za aina yoyote za kemikali.

Mohammed Javad Zarif amesema hayo leo hapa mjini Tehran wakati alipoonana na Ahmet Üzümcü, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali na kuongeza kuwa, Iran ni moja ya wahanga wa silaha za kemikali zilizotomiwa na utawala wa Saddam katika vita vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran. 

Ameongeza kuwa, kundi lolote lile halina haki ya kutumia silaha za kemikali vitani lakini inasikitisha kuona kuwa genge la kigaidi la Daesh linatumia silaha za kemikali katika vita vyake na serikali ya Syria.

Dk Mohammed Javad Zarif (kulia) akiwa katika mazungumzo Ahmet Üzümcü, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali

 

Vile vile amegusia ripoti ya hivi karibuni ya kutumiwa silaha za kemikali katika eneo la Khan Sheikhun nchini Syria na kusema kuwa, kuna wajibu wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na madai ya kutumiwa silaha hizo katika eneo hilo na kwamba Iran iko tayari kushirikiana na Shirika la Kuzuia Silaha za kemikali kufanya uchunguzi huo.

Kwa upande wake, Ahmet Üzümcü, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kuzia Silaha za Kemikali ameishukuru Iran kwa ushirikiano wake na shirika hilo na kuongeza kuwa, shirika lake linayafanyia uchunguzi madai ya kutumiwa silaha za kemikali katika eneo la Khan Sheykhun la kaskazini mwa Syria.

Tarehe 4 Aprili 2017, magenge ya kigaidi yalidai kuwa jeshi la Syria lilitumia silaha za kemikali katika eneo la Khan Sheykhun mkoani Idlib. Marekani ilitegemea madai hayo ya magenge ya kigaidi kushambulia kwa makombora kituo cha jeshi la anga cha Syria mkoani Homs bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa na kabla ya hata kuthibitishwa iwapo madai hayo ya magenge ya kigaidi ni kweli au ni uongo.