Jeshi la Iran: Ndege iliyoanguka mapema leo nje ya Tehran ilikuwa ya mizigo + Video
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa taarifa kuhusu ajali ya ndege iliyotokea mapema leo asubuhi karibu ya mji wa Karaj nje ya Tehran na kusema kuwa, ndege hiyo aina ya Boing 707 ilikuwa ya mizigo na ilikuwa ikitokea Bishkek Kyrgyzstan.
Kwa mujibu wa jeshi hilo, ndege hiyo imelazimika kutua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Fat'h mkoani Alborz, magharibi mwa Tehran na kupata ajali wakati wa kutua.
Msemaji wa taasisi ya uokoaji ya Iran amesema kuwa watu 16 walikuwemo kwenye ndege hiyo. Amesema muhandisi wa ndege hiyo tu ndiye aliyeokoka.
Mkuu wa mkoa wa Alborz, Azizullah Shahbazi amesema kuwa, ndege hiyo iliyokuwa imebeba mzigo wa nyama ilipata ajali baada ya kuondoka katika njia yake wakati ilipokuwa ikitua kwa dharura.
Ameongeza kuwa ndege hiyo ni mali ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini ilikuwa imeajiriwa na sekta ya watu binafsi.
Kamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Meja Jenerali Abdur Rahiim Mussawi amesema askari kadhaa wa jeshi hilo ni miongoni mwa walioaga dunia katika ajali hiyo.