Feb 11, 2019 14:24 UTC
  • Rais Rouhani: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaomba ruhusa kwa mtu yeyote ya kuunda zana za ulinzi + Picha

Rais Hassan Rouhani amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiombi na wala haitaomba ruhusa kwa mtu yeyote ya kuunda aina mbali mbali za makombora na zana za ulinzi; na itaendelea kufuata njia yake kwa nguvu na uwezo kamili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya mwaka wa 40 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipohutubia umati wa mamilioni ya wananchi waliofurika kwenye mnara wa Uhuru hapa mjini Tehran. Rais Rouhani amesisitiza kwa kusema: Dunia nzima ijue kwamba, nguvu na uwezo iliona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo hii ni mkubwa zaidi mara kadhaa kuliko ilivyokuwa katika zama za Kujihami Kutakatifu; na vikosi vya ulinzi vya Iran vinajitosheleza katika uundaji wa anuai za silaha na zana za kijeshi.

Rais Rouhani akiuamkia umati mkubwa wa wananchi katika mnara wa Uhuru

Rais Rouhani ameashiria ujasiri na moyo wa ushujaa vilionao vikosi vya ulinzi katika kuilinda nchi na kueleza kwamba: Walimwengu wameona jinsi wananchi wa Syria, Iraq na Lebanon walivyopata ushindi kutokana na irada na msaada wa Iran; na huko Palestina na Yemen pia muqawama wa kukabiliana na maghasibu na wavamizi ungali unaendelea.

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa: Leo maadui wamelazimika kukiri kuwa wameshindwa katika uingiliaji wao wa miaka 20 katika eneo na kuanza kuondoka kidogo kidogo ili mataifa ya eneo hili yaweze kuendeleza kwa uhuru njia yao ya ustawi na maendeleo.

Rais Rouhani (aliyevaa kilemba cheupe) katika maandamano ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amebainisha kwamba: Mahudhurio makubwa mno na yaliyofana ya wananchi katika maandamano ya kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yamethibitisha kuwa njama za maadui zimegonga mwamba na wala hawataweza katu kufikia malengo yao; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kufuata njia yake kama ilivyofanya kwa muda wa miaka 40 iliyopita.

Licha ya kunyesha mvua kubwa na theluji katika baadhi ya mikoa, wananchi wamejitokeza kwa wingi mno katika maandamano ya leo

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Dakta Rouhani ameashiria maendeleo iliyopata Iran katika nyuga mbali mbali ikiwemo ya petrokemikali na kueleza kwamba: Dunia nzima inakiri kuhusu maendeleo ya kasi iliyopata Iran. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, kuwa na nafasi Uislamu, wananchi yaani Jamhuri na kufanyika chaguzi za kuwachagua viongozi ni miongoni mwa matunda na mafanikio muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../

Tags