Rais wa Iran: Mustakabali wa eneo hili utaamuliwa na wanamapambano, sio meza ya mazungumzo
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kitakachoamua mustakabali wa eneo la Asia Magharibi na Palestina sio meza za mazungumzo na makubaliano kama yale ya "Oslo", "Camp David" na" Muamala wa Karne", bali muqawama na mapambano ya mataifa ndiyo yatakayoamua na kupanga utaratibu mpya wa kanda hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais wa Syria, Bashar al-Assad na ujumbe anaofuatana nao mjini Tehran kwa ajili ya kuwakumbuka mashahidi wa muqawama wa Syria na Iran akiwemo Jenerali Qassem Soleimani. Amesema Mujahidina wa muqawama wamethibitisha kuwa wao ni nguvu ya kutegemewa kwa ajili ya kuimarisha utulivu na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia ikiwemo Syria.
Akisisitiza ulazima wa nchi zote kuheshimu mamlaka na ardhi yote ya Syria, Raisi amesema: "Iran ilisimama upande wa wananchi na serikali ya Syria wakati baadhi ya viongozi wa Kiarabu na wasio Waarabu katika eneo hili walipokuwa wakiweka dau kuhusu wakati wa kuanguka kwa serikali ya Syria."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza masikitiko yake kwamba maeneo muhimu ya ardhi ya Syria bado yanakaliwa kwa mabavu na wanajeshi wa kigeni na kuongeza kuwa: Ardhi yote ya Syria lazima ikombolewe kutoka kwenye mikono michafu wa wavamizi ajinabi.
Raisi pia amesisitiza ulazima wa kuimarishwa ushirikiano na uratibu kati ya Iran na Syria katika masuala yenye maslahi ya pande zote mbili na kimataifa. Amesema, nia na hamu kubwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuboresha kiwango cha ushirikiano na uhusiano na Damascus hususan katika nyanja za kiuchumi na kibiashara.
Kwa upande wake, Rais Bashar al-Assad wa Syria pia amezungumzia nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia na kueleza kuwa, nchi yake iko tayari kwa ajili ya uratibu na ushirikiano wa kina na Iran katika nyanja za usalama, siasa na uchumi.
Bashar al-Assad ameutaja uhusiano wa Syria na Iran kuwa wa kistratijia na akasema: "Maendeleo katika kanda hii baada ya muongo mmoja wa vita dhidi ya muqawama yameonyesha kuwa kusimama kidete kuna matunda na taathira mzuri."
Akiishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na misaada na uungaji mkono wake kwa watu wa Syria katika vita dhidi ya ugaidi, Rais wa Syria amesema: Katika miaka ya mapambano na kukabiliana na hujuma za Wamagharibi na makundi ya kitakfiri, Iran ilikuwa nchi pekee iliyosimama upande wa Syria tangu mwanzo, na wananchi na serikali ya Syria wanalishukuru taifa la Iran na wanajiona kuwa wana deni kwa Jamhuri ya Kiislamu."