May 23, 2023 13:33 UTC

Rais Ebrahim Raisi amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Indonesia zimeamua kufanya mabadilishano ya kibiashara kwa kutumia sarafu zao za taifa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yuko ziarani nchini Indonesia kwa mwaliko rasmi wa rais wa nchi hiyo Joko Widodo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Rais Ebrahim Raisi ameeleza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Rais Joko Widodo wa Indonesia kuhusu malengo yaliyowekwa ya kufikisha kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi mbili hadi kufikia dola bilioni 20 ya kwamba, Tehran na Jakarta zimeamua kufanya mabadilishano hayo kwa kutumia sarafu zao za taifa.
Seyyid Ebrahim Raisi ameendelea kubainisha kuwa, kwa hima ya wataalamu wake vijana, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua zenye thamani kubwa katika mwelekeo wa ukuaji wa sayansi na teknolojia na maendeleo ya kiuchumi licha ya mashinikizo na vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa; na akasema: vikwazo na vitisho havijaweza kuisimamisha Iran kwa namna yoyote ile.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kueleza kwamba ushirikiano na mawasiliano na nchi za Kiislamu, nchi jirani na zenye mitazamo inayofanana ni kipaumbele cha siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akabainisha kuwa, kupanua uhusiano na Indonesia ikiwa ni moja ya nchi muhimu na athirifu barani Asia na duniani ni muhimu sana kwa Iran.
Rais Ebrahim Raisi (kushoto) akiamkiana na mwenyeji wake Rais Joko Widodo

Seyyid Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa Iran na Indonesia zina mitazamo ya pamoja kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa na akabainisha kuwa nchi hizo mbili zimeshikamana na msimamo thabiti katika kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina hadi Quds tukufu itakapokombolewa na zina mtazamo mmoja pia kuhusiana na udharura wa kuundwa serikali pana na jumuishi nchini Afghanistan inayowakilisha makabila na madhehebu zote na kuchukua hatua za kudhamini haki za watu wote wa nchi hiyo.

Wakati huohuo hafla ya utiaji saini hati za ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Indonesia imefanyika mjini Jakarta leo ambapo maafisa wa nchi hizo mbili wametia saini hati 11 za ushirikiano.
Makubaliano ya biashara ya upendeleo, kuondolewa kwa viza, mabadilishano ya kiutamaduni, ushirikiano katika usimamizi wa uzalishaji wa bidhaa za dawa, ushirikiano katika nyanja za sayansi, teknolojia na uvumbuzi, na ushirikiano wa nchi mbili katika sekta za mafuta na gesi, ni miongoni mwa hati za ushirikiano zilizotiwa saini kati ya mawaziri wa mambo ya nje, mawasiliano na teknolojia ya habari wa Iran na wenzao wa Indonesia.../

Tags