Jun 01, 2023 06:21 UTC
  • Amir Abdollahian:Kushiriki katika makongamano ya kimataifa ni moja ya hatua za sera za kigeni za serikali ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaja ushiriki chanya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika makongamano ya kimataifa kuwa moja ya hatua za doktrini za sera za nje zenye mlingano za serikali ya Iran.

Hossein Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi ameelekea Cape Town Afrika Kusini kwa lengo la kushiriki katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Rafiki za kundi la BRICS. Hii ni ziara ya tatu ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran barani Afrika. Kuhusiana na suala hilo, shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Hossein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika kukaribia safari yake nchini Afrika Kusini kwa lengo la kushiriki katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la BRICS huko Cape Town ameandika katika ukurasa wake wa twitter kwamba: BRICS inawakilisha nusu ya idadi ya watu duniani, ikiwakilisha takriban moja ya tano ya uchumi wa dunia. 

Amir Abdollahian ameongeza kuwa: Ushiriki chanya katika makongamano ya kimataifa ni moja ya hatua za doktrini za sera za nje zenye mlingano za serikali ya Iran.  Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wanachama wa kundi la BRICS unaanza leo Juni Mosi katika mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ambaye ni mwenyeji wa mkutano huu amewaalika Mawaziri wa Nchi zinazoomba uanachama katika kundi la BRICS akiwemo Amir Abdullahian kushiriki katika mkutano wa marafiki wa kundi hilo. Mkutano huo wa Cape Town utakuwa utangulizi wa mkutano ujao wa viongozi wa nchi za BRICS. 

Nchi wanachama wa BRICS 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mbali na kushiriki katika Mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa BRICS na nchi rafiki za kundi hilo; atakuwa pia na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi mwenyeji na pia Mawaziri wengine kadhaa wa Mambo ya Nje wanaoshiriki mkutano huo. Mawaziri hao watabadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya pande mbili.  

Kundi la BRICS linajumuisha nchi zinazoibukia kiuchumi duniani, yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, ambazo zinaunda takriban nusu ya watu wote duniani.

Tags