Jun 02, 2023 02:13 UTC
  • Iran na Afrika Kusini zatilia mkazo kustawisha uhusiano baina yao katika nyanja zote

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Afrika Kusini wamekutana pambizoni mwa kikao cha kundi la BRICS na kutilia mkazo wajibu wa kustawishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumatano usiku alielekea mjini Cape Town, Afrika Kusini kwa mwaliko wa nchi hiyo wa kushiriki kwenye kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la BRICS.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema, Amir-Abdollahian jana Alkhamisi alionana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Afrika Kusini, Bi Naledi Pandor na kusema kuwa, mfumo wa utawala duniani unaendelea kubadilika na kwamba jumuiya za Shanghai na BRICS zinaweza kuchangia mno katika kupatikana mfumo mpya wa nguvu za utawala ulimwenguni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia namna Tehran ilivyo na uzoefu mzuri wa kuzisaidia nchi jirani kupambana na vitendo vya kigaidi na ameipongeza Afrika Kusini kwa msimamo wake imara wa kuliunga mkono taifa la Palestina.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Bi Naledi Pandor amesema katika mazungumzo hayo ya ana kwa ana kwamba, anakaribisha kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga zote na kusisitiza kuwa, ugaidi ni katika hatari kubwa zinazolikabili eneo la kusini mwa Afrika hivi sasa.

Kikao cha siku mbili Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la BRICS kinafanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini. Wanachama waanzilishi wa kundi hilo ni Brazil, Russia, India na China ambazo zina uchumi unaokuwa kwa kasi kubwa.

Asilimia 30 ya ardhi ya dunia imo mikononi mwa nchi wanachma wa kundi hilo ambazo zinadhamini robo nzima ya uwekezaji duniani.

Tags