Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudia wakubaliana kuunda kamati za pamoja za kisiasa na kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98914-mawaziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_na_saudia_wakubaliana_kuunda_kamati_za_pamoja_za_kisiasa_na_kiuchumi
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia wamekubaliana kuunda kamati za pamoja za kisiasa na kiuchumi kati ya nchi mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2023 01:06 UTC
  • Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudia wakubaliana kuunda kamati za pamoja za kisiasa na kiuchumi

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia wamekubaliana kuunda kamati za pamoja za kisiasa na kiuchumi kati ya nchi mbili.

Hossein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mwenzake wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan jana walikuwa na mkutano na waandishi wa habari hapa Tehran. Katika mkutano huo, Amir Abdollahian alisema, wamekubaliana juu ya umuhimu wa kuunda kamati za pamoja za kisiasa, kuhusu masuala ya mipaka na kiuchumi na kupambana na magendo ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kushirikiana pande mbili katika suala la mazingira. 

Faisal bin Farhan (kushoto) katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran na mwenyeji wake Amir Abdollahian 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha ameeleza kufurahishwa na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia hapa Tehran na kusema: Ubalozi na balozi ndogo za nchi mbili hapa Tehran, huko Riyadh, Jeddah na Mash'had zitafunguliwa upya na mabalozi wa nchi hizo mbili wametambuliwa na majukumu yao  ya kisiasa yanatekelezwa. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesisitiza kuwa, Iran na Saudi Arabia zina mtazamo wa pamoja kuhusu suala la kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina. 

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia pia amesema: Tunafanya juhudi ili hatua za kidiplomasia ziendelee na sasa tunashuhudia ubalozi, ubalozi mdogo na ofisi ya uwakilishi ya Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zikiwa zimefunguliwa; na ubalozi wa Saudia nchini Iran utafunguliwa hivi karibuni.  

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia ameshukuru hatua ya Iran ya kuwezesha kufunguliwa tena ubalozi wa Saudia mjini Tehran na akasema: Ni muhimu kurejea uhusiano wa pande mbili katika hali ya kawaida kwa sababu pande zote mbili ni wahusika muhimu katika eneo. Amesema Uhusiano huu umejikita katika msingi mkuu wa kuheshimiana pande mili, kuacha kuingilia masuala ya ndani ya upande wa pili na kuheshimu hati ya Umoja wa Mataifa.   

Bin Farhan aidha amesema na hapa ninamnukuu:" Nataraji kuwa  kurejeshwa uhusiano wa nchi mbili kutakuwa na athari chanya kwa eneo zima na kwa ulimwengu wa Kiislamu; jambo ambalo litasaidia usalama wa kikanda na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi, kiutamaduni na katika nyanya nyinginezo.