Abdollahian: Kuimarisha uhusiano na majirani, kipaumbele cha Iran
(last modified Thu, 22 Jun 2023 07:28:01 GMT )
Jun 22, 2023 07:28 UTC
  • Abdollahian: Kuimarisha uhusiano na majirani, kipaumbele cha Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inalipa uzito suala la kuimarisha uhusiano na ushirikiano na mataifa jirani katika eneo la Asia Magharibi.

Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana Jumatano jijini Kuwait City, katika mazungumzo yake na Ahmad Nawaf Al Ahmad Al Sabah, Waziri Mkuu wa Kuwait na kusisitiza kuwa, sera ya nje ya Iran inatoa kipaumbele kwa masuala ya kuimarisha uhusiano na majirani zake.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Kuwait zina nafasi ya kuimarisha na kupiga jeki ushirikiano wao katika nyuga mbali mbali hasa za uchumi, biashara, usalama na siasa.

Kadhalika Amir-Abdollahian ametoa pendekezo la kuundwa Bunge la Kieneo litakalozileta pamoja nchi zinazopakana na eneo pana la Ghuba ya Uajemi, kwa upande wa kaskazini na kusini.

Kwa upande wake, Ahmad Nawaf Al Ahmad Al Sabah, Waziri Mkuu wa Kuwait amesema uwepo wa raia 30,000 wa Iran katika nchi hiyo ya Kiarabu ni sababu kuu ya kuimarika uhusiano wa ujirani mwema baina ya mataifa haya mawili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran jana Jumatano alielekea Kuwait baada ya mazungumzo na mashauriano kuhusu uhusiano wa pande mbili na viongozi wa Oman mjini Muscat. 

Aidha mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amewasili Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu mapema leo Alkhamisi katika mkondo wa nne wa safari yake ya kiduru ya kuzitembelea nchi za eneo hili la kistratejia.