Aug 24, 2023 02:32 UTC
  • Athari haribifu za kisaikolojia kwa wasichana wanaozuiwa kuendelea na masomo nchini Afghanistan

Madaktari wa masuala ya akili na saikolojia nchini Afghanistan wametoa tamko la kutisha linaloonesha ongezeko la wagonjwa wa akili hasa kati ya wasichana na uchunguzi wa madaktari hao unaonesha kuwa, kuzuiwa wasichana kuendelea na masomo kunachangia sana hali yao mbaya ya kisaikolojia, kujiona duni na kukata tamaa na msongo wa mawazo nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Shafaqna, madaktari hao wa masuala ya kiakili na kisaikolojia wa Afghanistan wanasema kuwa, hivi sasa wanapokea idadi kubwa ya wanawake na wasichana wenye matatizo ya akili. Gazeti la Washington Post nalo limeandika katika ripoti yake kuhusu uchunguzi wa wagonjwa wa akili Afghanistan kwamba, sehemu kubwa ya wagonjwa wa akili wanaosajiliwa katika hospitali za nchi hiyo ni wasichana na wanawake ambao wengi wanashtakia matatizo ya upweke, msongo wa mawazo, kutojiamini na mashinikizo ya kiakili.

Hayo ni sehemu ndogo tu ya matatizo na migogoro inayotokana na kuzuiwa kuendelea na masomo wasichana wa Afghanistan. Wasichana hao wamechoka kukaa majumbani bila ya kazi na kundi la Taliban hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi zake za kuandaa mazingira salama ya kuendelea na masomo wasichana hao kama walivyoahidi. Akram Arefi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema:

Kuzuiwa wasichana wa Afghanistan kuendelea na masomo ya juu ni pigo lisilofidika kwa jamii ya nchi hiyo ambayo mwanamke ndiye mama na baba wa familia

 

"Wakuu wa Taliban mara kwa mara huwa wanatoa ahadi za kuandaa mazingira mazuri ya kuendelea na masomo wasichana wa Afghanistan ili kupunguza mashinikizo ya ndani, ya kieneo na kimataifa dhidi yao, lakini viongozi hao hawatekelezi ahadi yoyote wanayoitoa na hali hiyo imepelekea kukata tamaa wasichana wengi wa Afghanistan na matokeo yake ni kuongezeka magonjwa ya kiakili na kuharibu usalama wa kiafya wa jamii ya akinamama nchini humo."

Matatizo ya kiakili na kisaikolojia ambayo ni sehemu ya majakamoyo yaliyotokana na kuzuiwa wasichana kuendelea na masomo huko Afghanistan, yameleta mgogoro mzito pia katika masuala ya kiuchumi na kijamii ya nchi hiyo. Baadhi ya familia zinalazimika kuhama nchi na kuhamia nchi nyingine zinazoruhusu wasichana kusoma. Zinazofanya hivyo ni familia zenye uwezo si za wananchi wa kawaida na wakati watu matajiri wanapohama nchi maana yake wanaondoka na fedha na mali zao kwenda kuzinufaisha nchi nyingine. Maana ya kuondoka wawekezaji nchini ni kuzorota mambo mengi yakiwemo masuala ya matibabu, huduma katika jamii na pia ushindani wa kufanya kazi. Kwa kweli kuzuia wasichana kuendelea na masomo kunatoa pigo kubwa kwa jamii ya madaktari na watu wa ofisini huko Afghanistan na madhara yake hayafidiki. Soroush Amiri, mtalamu wa masuala ya Afghanistan anasema:

"Kwa zaidi ya miongo minne sasa jamii ya Afghanistan imeghiriki katika matatizo na migogoro ya kila namna. Mbali na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mbali na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu nchi yao, wananchi wa nchi hiyo wamekumbana na matatizo mengine mengi katika kipindi hiki cha miongo minne kiasi kwamba hata mustakbali wa kizazi cha Afghanistan umeingia hatarini. Katika mazingira kama hayo, jamii ya Afghanistan imeongezewa mashinikizo mengine kwa kupigwa marufuku wasichana wasiendelee na masomo na sehemu muhimu sana ya jamii yaani wasichana na wanawake imetupwa na hivi sasa ina matatizo ya kiakili na kisaikolojia. Jamii ya Afghanistan haiwezi kustahamili mashinikizo zaidi hasa kwa kuzingatia kuwa wanawake wa Afghanistan ndio wasimamiaji wa familia kutokana na vita vya muda mrefu na kutokana na wanaume wengi kuuawa vitani. Kuwanyima elimu wanawake katika jamii kama ya Afghanistan ni pigo kubwa kwa jamii hiyo."

Viongozi wa Taliban mara kwa mara wanatoa ahadi za kuruhusu wasichana kusoma, lakini hawatekelezi

 

Alaakullihaal, baada ya kupita muda, athari mbaya za kupigwa marufuku wasichana kuendelea na masomo huko Afghanistan zitadhihirika zaidi. Hasara ya jambo hilo haifidiki. Kwa mtazamo wa jamii ya madaktari wa Afghanistan, kuongezeka matatizo ya kiakili na kisaikoljia kwenye jamii ya nchi hiyo si kitu chepesi cha kuweza kutatuliwa kiurahisi kwani kinahusu mustakbali wa kizazi cha sasa na cha baadaye nchini humo. Kinachohojiwa zaidi ni kwamba, kama unamzuia mtoto wa kike asisome, nafasi nyeti na muhimu kama za madaktari wa masuala ya uzazi na matatizo ya akinamama yatashughulikiwa na nani?

Inaonekana viongozi wa Taliban wanalielewa hivyo ndio maana taarifa zinazotolewa mara kwa mara zinaonesha kuwa, watoto wa kike wa viongozi hao wa kundi la Taliban wako katika nchi kama za Pakistan na Qatar wakijipiinda kwa elimu za kisasa kwa uhuru kamili. Aidha baada ya kuongezeka mashinikizo ya ndani, ya kieneo na kimataifa, hivi karibuni viongozi wa Taliban nchini Afghanistan walirudia kusema kuwa watarekebisha mfumo wa masomo ili wasichana waweze kuendelea na masomo yao lakini kwa kuwa ahadi hizo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara bila ya kutekelezwa, ahadi za hivi sasa pia zitazidisha tu kukata tamaa na matatizo ya kisaikolojia kwa akinamama na wasichana wa Afghanistan. Njia pekee ya kufanya ni kundi la Taliban kufanya haraka kufungua shule kwa wasichana na kuruhusu akinamama kufanya kazi ili kupunguza msongo wa mawazo na matatizo mengi ya kisaikolojia na kiakili waliyo nayo hivi sasa.

Tags