Sep 24, 2023 10:54 UTC
  • Hamas yaishukuru Afrika Kusini kwa kuwaondolea visa Wapalestina

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeishukuru serikali ya Afrika Kusini kwa kuwaondolea visa Wapalestina.

Jana Jumamosi, serikali ya Afrika Kusini ilitangaza kuwa, imeamua kuwaondolea visa ya kuingia nchini humo Wapalestina wote ikiwa ni sehemu ya uungaji mkono wake kwa malengo matukufu ya muqawama wa Palesitna na mapambano yao dhidi ya utawala vamizi wa Kizayuni. 

Serikali ya Afrika Kusini imesema pia kuwa, imechukua hatua hiyo ili kutangaza uungaji mkono wake kwa juhudi za kimataifa za kuhakikisha kunaundwa nchi huru ya Palestina na kusema kwamba, Mpalestina yeyote mwenye pasi ya kusafiria ya Palestina anaruhusiwa kuingia nchini humo bila ya visa kutoka ubalozi wowote wa Afrika Kusini.

Bango linaloonesha uungaji mkono mkubwa wa Afrika Kusini kwa muqawama wa Palestina

 

Shirika la habari la Palestina SAMA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, leo Jumapili, Harakati ya Mapambano ya Palesina HAMAS imetoa taarifa na kuishukuru serikali ya Afrika Kusini kwa hatua nzuri iliyochukua ya kuwaondolea visa Wapalestina na kutangaza mshikamano wake na wanamuqawama wa Palestina wanaopigania ukombozi wa ardhi zao.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema kuwa, ujumbe wa hatua hiyo ya kuondolewa visa Wapalestina wanaoingia nchini humo ni kutangaza mshikamano mpya baina ya serikali na wananchi wa Afrika Kusini kwa taifa la Palestina na kuonesha kuwa, taifa la Afrika Kusini daima liko katika mapambano dhidi ya ukoloni, ukandamizaji na ubaguzi wa rangi na kizazi.

Misimamo ya serikali ya Afrika Kusini siku zote ni mizuri na ya kupigiwa mfano kuhusu kadhia ya Palestina na ukombozi wake.