Watoto wa Kipalestina; wahanga wakuu wa siasa za jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza
Kanali ya Al-Arabi imeripoti kwamba zaidi ya asilimia 70 ya watoto wa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na matatizo mengi ya kiafya na kimwili yakiwemo ya upungufu wa damu.
Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, takriban asilimia 73 ya wakazi wa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na uhaba wa chakula, na zaidi ya nusu yao wanaishi chini ya mstari wa umaskini, hali ambayo inapunguza uwezo wao wa kujidhaminia chakula na virutubisho muhimu.
Watoto wa Ukanda wa Gaza, wamekuwa wakipitia wakati mgumu na mchungu kwa miaka mingi.
Kutokana na hali ngumu ya eneo linalozingirwa la Ukanda wa Gaza, akina mama na watoto wanakabiliwa na changamoto kubwa, mojawapo ikiwa ni utapiamlo ambao una athari kubwa hasi kwa watoto ikiwemo ya kuongeza hatari ya wao kupata magonjwa ya mara kwa mara.
Kwa miaka mingi sasa utawala wa Kizayuni umekuwa ukiwanyima watoto na watu wanaougua maradhi yasiyotibika katika Ukanda wa Ghaza kuendelea na matibabu nje ya eneo hilo, na kwa sababu hiyo wagonjwa wa eneo hilo linalozingirwa na Wazayuni wanakabiliwa na hatari ya kifo cha taratibu.
Utawala wa Kizayuni umekiuka pakubwa haki za watoto wa Kipalestina na wala hauzingatii hata moja ya mikataba ya haki za watoto.
Sekta ya afya huko Gaza inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vifaa vya matibabu na dawa, na suala hili limekuwa na athari nyingi mbaya kwa maisha ya wagonjwa, hasa watoto.

Vita vitatu mfululizo vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza vimesababisha uharibifu wa aghalabu ya vifaa vya matibabu vya hospitali za ukanda huo au kuvipelekea visifanye kazi vizuri.
Tangu ushindi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika uchaguzi wa kitaifa wa mwaka 2006, utawala wa Kizayuni umelizingira eneo hilo lenye watu zaidi ya milioni 2 na kuligeuza kuwa jela kubwa zaidi ya wazi duniani, ambapo watoto ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi ya jinai hiyo, kwa kutoa roho zao.
Katika uchaguzi wa 2006 ambao uliambatana na ushiriki wa asilimia 77 ya wananchi, harakati ya Hamas iliweza kushinda viti 76 kati ya viti vyote 132 vya Bunge la Palestina.
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, watoto wa Kipalestina ndio wahanga wakuu wa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni, ambapo zaidi ya watoto laki nane huko Gaza wamekuwa chini ya mzingiro tangu wazaliwe.
Mzingiro huo umewanyima watu wa eneo hilo haki zao za msingi, yaani haki ya kuishi, kupata huduma za matibabu, usafiri na elimu, tangu miaka 17 iliyopita, na hilo limekuwa likichangiwa pakubwa na kimya cha taasisi za kimataifa.
Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, kiwango cha uhaba wa ajira katika Ukanda wa Gaza ni kikubwa sana ambapo mwaka uliopita wa 2022, kiwango hicho kilifikia asilimia 46.6, kiwango cha uhaba wa ajira kati ya vijana wenye umri wa miaka 15-29 kati ya idadi hiyo kikiwa cha juu zaidi kwa kufikia asilimia 62.5.
Mbali na madhara ya mzingiro huo, uharibifu wa kimpangilio unaofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya miundombinu ya Ukanda wa Gaza wakati wa hujuma zake za mara kwa mara katika ukanda huo umeathiri vibaya hali yake ya kiuchumi ambapo sekta nyingi za viwanda zimeharibiwa.
Kuzingirwa Ukanda wa Gaza na utawala wa Kizayuni kumesababisha hasara kubwa katika mifumo ya miundombinu, nishati, umeme na pia sekta ya afya, na wala utawala huo hauruhusu huduma za matibabu kutolewa ndani na nje ya ukanda huo.
Kuwa na afya bora na elimu ni miongoni mwa haki za kimsingi za kila mwanadamu na sheria na mikataba yote ya kimataifa inasisitiza haki hiyo, lakini Wapalestina wamenyimwa haki hiyo ya wazi na wala hakuna yeyote duniani anayewatetea kuhusu suala hilo.
Jamii ya kimataifa haichukui hatua zozote za kusimamisha mzingiro na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Ukanda wa Gaza, na la kusikitisha zaidi ni kuwa hivi karibuni misaada ya kibinadamu kwa ukanda huo pia imepungua.
Utawala wa Kizayuni unatekeleza kwa makusudi siasa za "kutokufa wala kuishi" dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza, ambapo unawanyima na kukiuka wazi haki zao za msingi zikiwemo za kuishi na kupata huduma za matibabu.
Vitendo hivyo vimewafanya Wapalestina zaidi ya milioni 2, hasa wanawake, watoto na wagonjwa wa saratani wanaohitaji matibabu ya mara kwa mara katika hospitali za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Beitul Muqaddas, kuwa mateka wa utawala ghasibu wa Israel.

Ili kupunguza kuharibika zaidi hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kuondoa kabisa vikwazo vinavyotekelezwa na utawala wa Kizayuni, hatua za kivitendo zinapaswa kuchukuliwa kwa lengo la kutekeleza kikamilifu azimio nambari 1860 la Baraza la Usalama lililopitishwa mwaka 2009.
Hali hiyo ya kusikitisha haiishii hapo, bali watoto na vijana wa Kipalestina mbali na kustahamili hali ngumu ya maisha inayosababishwa na vikwazo hivyo vya kikatili, wanatatizika hadi kufa kutokana na mashambulizi makali ya jeshi la Kizayuni.
Majina ya kwanza ya watoto wa Kipalestina waliouawa na utawala wa Kizayuni yalisajiliwa Novemba 1950, wakati watoto wa Kipalestina wa miaka 8, 10 na 12 kutoka kijiji cha Yalo karibu na Deir Ayyub walipigwa risasi bila huruma.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, watoto 77 wa Kipalestina waliuawa shahidi mwaka 2021 pekee, ambapo idadi hiyo imeongezeka hadi zaidi ya watoto 2,200 tangu 2000.
Pia mwaka 2021, kati ya watoto 500 hadi 700 walihukumiwa katika mahakama za kijeshi za utawala wa Kizayuni. Watoto wanaozuiliwa katika jela za Kizayuni wananyimwa haki za masomo, huduma za matibabu na mawasiliano na familia zao. Familia za watoto hao zimepigwa marufuku kuwapelekea nguo, matumizi binafsi na vitabu vya kiutamaduni, na wala uongozi wa gereza huwa hausiti kuwachukulia hatua kama inavyowachukulia wafungwa watu wazima kwa kuvamia vyumba vyao, kuwarushia mabomu ya kuoa machozi, kuwapiga na kuwatesa kimwili.
Baada ya kuundwa serikali ya itikadi kali na ya mrengo wa kulia ya Netanyahu, mateso hayo dhidi ya wafungwa watoto yameongezeka kwa kiwango cha kutisha. Hii ni kwa sababu mateso yoyote makali dhidi ya Wapalestina na watoto wa Kipalestina huungwa mkono kikamilifu na baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni na hivyo kupata sura ya kisheria kabisa.