Sep 26, 2023 02:51 UTC
  • Kushadidi jinai za Utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza

Wanajeshi wa Kizayuni wameushambulia mji wa Tulkarem katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwaua shahidi vijana wawili wa Kipalestina.

Mashambulizi ya Jumapili  ya askari wa Kizayuni katika kambi ya Nour Shams huko Tulkarem ambayo yaliochukua takriban masaa 5 na kuhusisha zaidi ya magari 100 ya kijeshi na mabuldoza ya kubomoa nyumba yalipelekea kuuawa shahidi vijana wawili wa Kipalestina na nyumba kadhaa za Wapalestina kuharibiwa. Idadi kadhaa ya askari vamizi wa Kizayuni pia walitumbukia kwenye mtego wa vijana wa Palestina na kujeruhiwa.

Wiki iliyopita pia Wazayuni waliwaua shahidi Wapalestina 7 na kujeruhi makumi ya wengine. Awali ripoti ya Taasisi ya Washington ilionyesha kuongezeka ghasia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na hilo linathibitishwa na takwimu zinazokusanywa na kutolewa katika eneo hilo.  Kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, Wazayuni 28 wameuawa na Wapalestina 137 kufa shahidi katika operesheni za muqawama wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu.

Inaonekana kuwa kuongezeka ghasia na vitendo vya mabavu dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kunatokana na nukta mbili kuu. Ya kwanza ni kuenea harakati za mugawama katika Ukingo wa Magharibi  katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, na kujiunga Waplestina wengi na harakati hizo. Utawala wa Kizayuni daima umekuwa ukijaribu kuzuia kuenea harakati za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, lakini kuimarishwa uhusiano wa baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala huo ghasibu na kuongezeka mashambulizi dhidi ya Wapalestina kumewapelekea kufikia natija kwamba mapambano ndiyo njia pekee ya kulinda na kutetea maslahi ya nchi yao ya Palestina. 

Eneo la Nour Shams Magharibi mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan

Kabla ya hapo, Wazayuni walikuwa wakikabiliana tu na mashambulizi ya Wapalestina wa kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na katika Ukanda wa Ghaza, lakini katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, eneo la  mashariki mwa Ukingo wa Magharibi limebadilika kuwa ngome ya mashambulizi ya vijana wa Kipalestina dhidi ya walowezi wa Quds. 

Nukta ya pili ni kwamba baraza la  mawaziri lenye  misimamo mikali  la Benjamin Netanyahu linaamini kwamba kutekelezwa siasa kali  dhidi ya Wapalestina, kunaweza kuwatia uwoga na hivyo kuzuia kuimarishwa kwa harakati za makundi ya mapambano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Baadhi ya mawaziri katika baraza hilo hususan Itmar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala huo wanatilia mkazo kuendelezwa siasa kali na za jinai dhidi ya Wapalestina. Pamoja na hayo, sera na siasa hizo za jinai si tu kwamba zimeshindwa kuzima moto wa mapambano ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, bali pia zimewaunganisha na kuwapa Wapalestina moyo na azma zaidi ya kukabiliana na siasa za kujitanua za utawala huo ghasibu wa Kizayuni.

Kuhusiana na hilo, baada ya mashambulizi ya Wazayuni huko Tulkarem, taasisi mbalimbali za kiserikali na za wananchi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huku zikisimamisha shughuli zao na kutangaza siku ya maombolezo, zimesisitiza juu ya kuendelea muqawama dhidi ya siasa za kichokozi za utawala huo ghasibu wa Kizayuni. Mundhir Al-Hayek, Msemaji wa harakati ya Hamas huko Tulkarem amesema kuwa kinyume na wanavyodhani Wazayuni siasa za  mauaji na uvamizi hazijafanikiwa kuvunja moyo na irada ya vijana wa Palestina katika kukabiliana na mashambulizi dhidi yao. Wakati huo huo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas)  imelaani vikali shambulio la karibuni la walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa na kulitaja shambulio hilo kuwa katika mwendelezo  wa mashambulio ya Wazayuni ambayo yanapandisha hamasa ya vijana wa Kipalestina katika kukabiliana na mashambulizi ya kikatili ya askari wa utawala ghasibu wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi zao.

 

Tags