Dec 02, 2023 04:19 UTC
  • Muqawama wajibu jinai za Israel; HAMAS yasema: Marekani na Israel ndio wa kulaumiwa

Muqawama wa Palestina umejibu jinai mpya za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza huku Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ikisema kuwa, wa kubebeshwa dhima na lawama za kuanza tena mapigano ni Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Televisheni ya Al Mayadeen imetangaza kuwa, Muqawama wa Palestina umeendelea kukabiliana kishujaa na vilivyo na uvamizi wa jeshi la Israel katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza hasa kwenye eneo la al-Tawam la kaskazini magharibi mwa mji wa Ghaza.

Jana asubuhi, utawala wa Kizayuni ulianzisha tena jinai zake za kuua kikatili na kwa umati watu wasio na hatia kwenye maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza, baada ya kukwamisha mazungumzo ya kuendeleza usimamishaji vita kati yake na HAMAS. 

Makumi ya wananchi wa Palestina wameuawa shahidi katika saa za awali tu za kuanza jinai hizo mpya hasa katika maeneo ya kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza jana Ijumaa.

Utawala wa Kizayuni umeanzisha upya jinai zake huko Ghaza kwa idhini ya Marekani

 

Kwa upande wake, Usama Hamdan, kiongozi mwandamizi na wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alisema jana jioni kuwa, utawala wa Kizayuni na Marekani ndio wanaopaswa kubebeshwa lawama zote za kuanza upya mashambulizi ya kinyama na kuendelea kuuliwa kidhulma wananchi wa Palestina.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kupita takriban siku 50 za mashambulio ya mfululizo ya jeshi katili la Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza, hatimaye kulianza kutekelezwa makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda wa siku nne kwa upatanishi wa Qatar.

Makubaliano hayo yaliongezewa muda kidogo kidogo na kufikia wiki moja huku utawala wa Kizayuni ukilazimika kutii matakwa ya wanamapambano wa Palestina hasa kusimamisha vita, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingia kwenye Ukanda wa Ghaza pamoja na mabadilishano ya mateka ambapo utawala wa Kizayuni ulilazimika kukubali masharti ya muqawama wa Palestina ya kubadilisha kila mateka watatu wa Palestina kwa mateka mmoja tu Mzayuni.