Dec 06, 2023 09:00 UTC
  • Israel kuanzisha tena vita kwailazimisha Yemen kuchukua hatua

Hatua ya baraza la mawaziri lenye misimamo mikali la Netanyahu kukataa kukubali usitishaji vita wa kudumu kumeigharimu pakubwa Israel sio tu katika kuongeza vifo vya wanajeshi wake katika vita vya nchi kavu, bali pia katika kufungua tena pande mpya za vita dhidi ya utawala huo wa kibaguzi kutoka kusini mwa Lebanon hadi Golan ya Syria na Yemen.

Hivi sasa utawala wa Kizayuni kwa upande mmoja unakabiliana na vikosi vya Qassam, tawi la kijeshi la Hamas lenye ujuzi mkubwa katika medani ya vita, na kwa upande wa pili na makombora ya Iraq na Syria na vile vile mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Hezbollah yanayovurumishwa katika eneo la kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu. Katika upeo wa baharini unakabiliwa na mashambulizi ya ushiriki hai wa wapiganaji wa Ansarullah ya Yemen ambao wanaendesha mashambulio dhidi ya utawala huo kwa ajili ya kuwasaidia wenzao wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na mashambulizi ya kinyama ya utawala huo.

Kama ambavyo hatua ya Ansarullah ya kukamata meli kadhaa za Israel kulichangia katika kuulazimisha utawala wa kigaidi wa Israel kukubali usitishaji vita wa muda, hatua ya utawala huo ya kuanzisha tena mashambulizi ya kinyama dhidi ya wakazi wa Gaza imevipelekea vikosi vya Yemen kuchukua tena hatua dhidi ya maslahi ya utawala huo ili kuulazimisha usimamishe mashambulio na kukubali usitishaji vita wa kudumu. Kwa kuzingatia kuwa Marekani unauunga mkono kijeshi na kifedha utawala huo haramu, jeshi na wapiganaji wa Ansarullah pia wameamua kuzilenga meli za Marekani ili kuifanya isitishe mauaji ya halaiki dhidi ya raia wa Gaza.

Jeshi la Yemen limesema katika taarifa iliyotangazwa na kanali ya televisheni ya Al-Masira kwamba ikiwa ni katika utekelezaji wa amri ya Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah, na kuitikia wito wa taifa la Yemen na watu huru wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, kwa ajili ya kuwatetea watu wa Palestina jeshi la nchi hiyo karibuni lilitekeleza oparesheni ya kulenga meli mbili za Israel huko Bab al-Mandab kwa majina ya Unity Explorer na Number Nine, ya kwanza ikilengwa kwa kombora la majini na ya pili ikilengwa kwa ndege isiyo na rubani. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya meli hizo kutozingatia jumbe za onyo za Jeshi la Wanamaji la Yemen.

Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi

Pia, kwa mujibu wa maafisa wa ulinzi wa Marekani, manowari aina ya USS Carney (DDG-64) imeshambuliwa katika Bahari ya Sham kwa makombora na ndege zisizo na rubani za Houthi magharibi mwa Yemen. Manowari ya Carney awali alihusika katika utunguaji wa makombora manne na ndege 15 zisizo na rubani zilizorushwa na Ansarullah kuelekea kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Mmoja wa viongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen akijibu matamshi ya afisa mmoja wa Marekani aliyesema kuwa Washington ina haki ya kujibu mashambulizi ya Ansarullah amesisitiza kuwa, Wamarekani hawana haki yoyote katika Bahari ya Sham hadi wadai kuwa wana haki ya kujibu mashambulizi hayo!

Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, ameandika katika akaunti yake ya mtandao wa "X" kwamba: "Wakati Marekani itakapokubali na kukiri uhalali wa kuwepo nyambizi ya Korea Kaskazini au manowari za kisasa za China za kubeba ndege za kivita karibu na Florida katika maji ya kimataifa, hapo ndipo na sisi tutakubali uwepo halali wa Marekani katika maji ya kimataifa ya Bahari ya Sham na hiyo ni baada ya kufanyika kura ya maoni nchini Yemen kuhusiana na suala hilo."

Vikosi vya jeshi la majini la Yemen awali vilionya kwamba vitaendeleza operesheni za kijeshi dhidi ya meli na maslahi ya adui wa Israel hadi hujuma zake dhidi ya Gaza na jinai dhidi ya taifa la Palestina zitakapokomeshwa.

Vikosi vya jeshi la Yemen pia vimetangaza kuwa vitalenga meli yoyote ya Israel itakayopatikana katika maji ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na hatua ya kijeshi ya utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu katika Ukanda wa Gaza.

Misimamo ya kivitendo ya jeshi la Yemen katika kipindi cha miezi miwili iliyopita imeliinua kihadhi jeshi hilo na kuthibitisha kuwa ni mwanachama mwenye nguvu na wa kutegemewa katika mhimili wa muqawama. Jeshi ambalo kwa upande mmoja limekuwa jinamizi kwa jeshi la Marekani katika eneo kwa mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani na makombora, na kwa upande mwingine, limevuruga pia uchumi wa utawala haramu wa Israel kwa kusimamisha usafiri wa meli zake za kibiashara katika lango la Bab al-Mandab katika Bahari Nyekundu (Sham).

Kwa kutilia maanani kuwa asilimia 85 ya biashara ya Wazayuni inafanyika kwa njia ya bahari na viongozi wa utawala huo wanaichukulia Bahari Nyekundu kuwa njia kuu ya kukidhi mahitaji yake ya kiuchumi, kuendelea operesheni za jeshi la Yemen katika eneo hilo kunaweza kutoaa pigo kubwa kwa utawala huo. Hii ni katika hali amabyo hali mbaya ya  uchumi wa utawala huo inazidi kudhihirika siku baada ya siku.

Meli ya kubeba mafuta

Kwa msingi huo, weledi wa mambo wanaamini kuwa, kurejea vitani utawala wa Kizayuni ni kosa kubwa la kistratijia, ambapo hivi sasa utawala huo si tu unalazimika kupigana na Hamas na Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, bali pia na pande nyingine zilizo nje ya mipaka ya Palestina, ambapo pande kadhaa mpya zimejitosa kwenye medani ya vita dhidi ya utawala huo. Pande hizo mpya bila shaka zitajiimarisha kijeshi kadiri vita vitakavyoendelea kupanuka. Mbali na hayo, kuendelea vita kunaweza kuongeza na kupanua upinzani wa kisiasa na wa maoni ya umma dhidi ya utawala huo na hasa dhidi ya waziri mkuu wake, Benjamin Netanyahu.